December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yafunguka takwimu za Corona

Na Mwandishi Maalum, WAMJW

SERIKALI imetaja sababu zilizosababisha kutotoa taarifa za takwimu za maabara kuhusu mwenendo wa Corona nchini kwa siku saba, huku ikiwataka wananchi waendelee kuchukua tahadhari kwani ugonjwa bado upo.

Hata hivyo imesema itaendelea kutoa takwimu za mwenendo kuhusu Ugonjwa wa Corona mara baada ya kukamilika kwa maboresho ya kiufundi ya Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akizindua kituo cha Afya cha huduma kwa wateja (Afya call center) kilichopo eneo la Chuo cha Afya ya Sayansi ya Jamii Muhimbili (MUHAS), upanga Dar es Salaam.

“Takribani siku saba sasa hatukuweza kutoa taarifa za takwimu za maabara kuhusu mwenendo wa Corona nchini kwa sababu sasa hivi tunafanya maboresho ya maabara ya taifa ya afya ya jamii hivyo niwatoe hofu wananchi kwamba ndani ya siku chache zoezi litakamilika na tutaendelea kutoa taarifa kwa umma mara kwa mara”, amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema, Corona ipo na itaendelea kuwepo kwa miezi kadhaa hivyo wananchi wanapaswa kujua namna ya kuishi na ugonjwa huo kwa kujikinga na maambukizi.