Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amezindua mafunzo ya umahiri wa ufundi simu za mkononi pamoja na mtaala wa mafunzo hayo.
Akizungumza jijini Dodoma na mafundi simu wanaotarajia kuanza mafunzo hayo katika Chuo cha Ufundi (VETA) ambako mafunzo hayo yanatolewa ,Akwilapo amewataka mafundi hao kuzingatia mafunzo yatakayotolewa ili wakafanye kazi yao kwa weledi na kujitengenezea ajira na uchumi wao,badala ya kufikiria kupata leseni na cheti pekee.
Vilevile amewataka kufikiria kujiendeleza zaidi baada ya kuhitimu mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwa wiki tano kwa ufadhili wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA).
“Teknolojia imekua,lakini pia kazi yenu inahitaji weledi mkubwa kwani chombo mnachokifanyia kazi ni zaidi ya mawasiliano,mnatakiwa kuwa weledi .” amesema Dkt.Akwilapo na kuongeza
“Lakini takwimu za mwaka 2012 zinaonyesha watumiaji wa simu za mkononi walikuwa milioni 17,takwimu za sasa zinaonyesha watumiaji hao wamefikia milioni 48.
Hii inaonyesha wazi kuwa jamii imeelewa matumizi ya mawasiliano na sauala zima la ukuaji wa uchumi kupitia sekta hiyo hivyo mnalo jukumu la kujiendeleza zaidi kwani wigo wa mawasiliano unaendelea kupanuka.”
Aidha ameyataka kampuni mengine yakiwemo makampuni ya simu za mkononi kuiunga mkono TCRA katika kufadhili mafunzo hayo kwa lengo la kupata wataalam wa kutosha katika sekta hiyo.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TCRA John Daffa amesema TCRA imeanzisha mitaala wa mafunzo simu ili kurasimisha shughuli za utengenezaji simu lakini pia kuepukana na changamoto mbalimbali ikiwemo kupunguza wimbi la wizi wa simu za mkononi.
Amesema kwa mkoani wa Dodoma jumla ya mafundi simu 100 wamepata fursa ya kupata mafunzo hayo kati ya 250 walioomba.
Amewataka mafundi hao waliopata nafasi kuitumia fursa hiyo vizuri ili waweze kuingia katika ushindani huku akisema baada ya kuhitimu sasa kutakuwa na mafundi wataalam ambao wamesomea kazi hiyo badala ya kufanya kazi kwa uzoefu na kusababisha wengi wao kuharibu simu za watu badala ya kutengeneza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA Mhandisi Pancras Bujulu amesema,mafunzo hayo yamelenga kuongeza tija na kuinua zaidi uchumi wa viwanda kupitia tehama.
Kwa upande wa wenyeviti wa mafundi simu kutoka mikoa ya Dodoma na Mwanza wamesema,mafunzo hayo yatawasaidia mafundi kufanya kazi zao kwa kujiamini na siyo kwa ujanja ujanja kama ilivyokuwa awali kabla ya kupatiwa mafunzo hayo.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani