November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yafungua fursa uwekezaji mazao ya samaki

Na Esther Macha,Timesmajira Online. Mbeya

KITUO cha Uwekezaji Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (TIC), kimesema kimefungua milango ya fursa za uwekezaji kwa kutenga maeneo ya uwekezaji wa kilimo cha mazao ya samaki wilayani Kyela Mkoa wa Mbeya.

Akizungumza Ofisa Uhamasishaji Uwekezaji Kanda, Ajelandro Sindano amesema licha ya kuwepo kwa fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya kilimo na sasa, wamefungua fursa za kilimo cha ufugaji wa samaki ambacho kina masoko ya uhakika.

Sindano amesema ni wakati sasa kwa wawekezaji kutumia Kituo cha TIC kama daraja la kuwaunganisha na serikali katika kutambua fursa za uwekezaji na kutatua changamoto mbalimbali zilizopo.

“Fursa ziko nyingi sana Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, hivyo ni wakati sasa kwa wawekezaji kutumia fursa hiyo hususan wazawa ili kuunga mkono jitihada za serikali, kuwekeza katika nyanja mbalimbali za kiuchumi,” amesema.

Ofisa huyo amesema, sekta ya uwekezaji nchini imekuwa chachu katika ukuaji wa uchumi na ndiyo sababu ya serikali, kuelekeza nguvu kwa kutaka kuzitangaza fursa zilizopo ili kuvutua watalii wengi na kuongeza mapato.

“Pia kuna utalii wa ndani ambao unachochea kupatikana kwa ajira kwa vijana, hivyo ni wakati sasa jamii kuona kuwa kuna umuhimu wa kutumia majukwaa kutangaza fursa zilizopo, ili kuvutia wawekezaji na watalii wa nje,” amesema.

Kwa upande wake mfanyabishara wa kusindika mazao ghafi, Kisa Atupele ameiomba TIC kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji mdogo ili kuwawezesha kuongeza tija ya uzalishaji.

Ameomba pia kuwepo kwa mifumo rafiki ya kuwaunganisha wawekezaji wadogo, wakubwa na wakati katika minyororo ya thamani ya mazao yanayowekezwa ili kuchochea sekta ya uwekezaji kupiga hatua na kunufaisha wengi.