Yatangaza bei elekezi kwa kila mkoa, wafanyabiashara watakaokaidi kufutiwa leseni, yataja changamoto zilizosababisha tatizo hilo
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga ametangaza ukomo wa kiwango cha juu cha sukari kwa bei ya rejareja kwa kila mkoa nchini.
Waziri Hasunga alitangaza bei elekezi ya sukari kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma akiwa na waziri mwenzake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa. Katika mkutano huo mawaziri hao walizungumzia kuhusiana na hali ya sukari nchini na mwenendo wa bei yake katika msimu huu wa uzalishaji wa sukari wa 2019/2020.
Sheria inayompa nguvu
Waziri Hasunga kabla ya kutangaza bei ya sukari ya rejareja katika mikoa yote nchini, alisema kwa mujibu wa Sheria ya Sukari Na. 26 ya Mwaka 2001 (Cap. 251) chini ya kifungu cha 11A inampa Mamlaka Waziri mwenye dhamana ya Kilimo kutangaza bei ya ukomo wa juu ya sukari.
Alisema kutokana na changamoto ya wafanyabiashara kupandisha kiholela bei ya sukari nchini, Serikali imeamua kuutangazia umma wa Watanzania kikomo cha bei ya sukari katika mikoa yote nchini Tanzania.
Bei inayodhibitiwa
Alisema bei hizo zinalenga kukabaliana na changamoto ya kupanda kiholela kwa bei ya sukari nchini ambayo kwa sasa imefikia wastani wa sh.4,000 hadi sh. 4,500 kwa kilo. Alisema bei hii kikomo ya sukari imepangwa kwa kuzingatia gharama zote za uagizaji wa sukari kuziba pengo linalotumiwa na wazalishaji kuagiza sukari kutoka nje ya nchi.
Bei elekezi
Alisema bei ya sukari ya reja reja katika mikoa yote nchini itakuwa ni kama ifuatavyo; Iringa sh. 2,900, Mbeya sh.3,000, Rukwa sh.3,200, Katavi sh. 3,200, Ruvuma sh. 3,200 na Njombe sh.2,900.
Bei elekezi ya mikoa mingine ni Lindi sh. 2,800, Mtwara sh.2,800 Arusha sh. 2,700, Kilimanjaro sh. 2,700, Manyara sh. 2,700, Tanga sh. 2,700, Dar es es Salaam 2,600, Pwani sh. 2,700, Morogoro sh.2,700, Kagera sh. Kagera 3,000, Mwanza sh. 2,900, Simiyu sh. 2,900, Shinyanga sh 2,900, Geita sh. 2,900, Mara sh. 3,000, Kigoma sh. 3,200, Singida sh. 2,900, Tabora sh. 2,900, Dodoma sh. 2,900 na Songwe 3,000,
Adhabu kwa watakaokaidi
‘‘Bei hizi za ukomo za sukari zimezingatia umbali wa kila eneo katika mikoa yote nchini.
Niwaombe wafanyabiashara wote nchini kuzingatia maelekezo haya ya Serikali. Yeyote atakayekiuka maelekezo haya atakuwa ametenda kosa na hivyo atafikishwa katika vyombo vya sheria ili apate adhabu ambayo itahusisha ama kunyang’anywa leseni ya biashara, kulipa faini au adhabu zote kwa pamoja,” alisema Waziri Hasunga na kusisitiza;
“Tutachukua hatua kali za kisheria kwa mfanyabiashara yeyote ambaye atakiuka masharti haya.’’
Mahitaji ya sukari
Waziri wa Kilimo, Hasunga alitumia mkutano huo kueleza mahitaji na matumizi ya sukari nchini akisema;
“Mahitaji ya sukari ya matumizi ya kawaida nchini yanakadiriwa kufikia tani 470,000 kwa Mwaka. Kiasi hiki ni kwa wastani wa mahitaji ya kiasi cha tani 38,000 kwa kila mwezi pamoja na kiasi cha tani 14,000 kwa ajili ya dharura.”
Uwezo wa viwanda
Alisema uwezo wa viwanda vya ndani kwa msimu wa 2019/20 kwa mujibu wa makadirio ya mwanzoni mwa msimu yaani Julai, 2019 ni kuzalisha takribani tani 378,000 za sukari. Alisema kiasi hicho ni sawa na asilimia 82.9 ya mahitaji halisi ya tani 456,000 ambayo hayajumuishi kiasi cha dharura cha tani 14,000.
Uwezo huu wa uzalishaji wa viwanda vya ndani unaacha pengo la kiasi cha tani 78,000 ili kuweza kutosheleza mahitaji halisi ya tani 456,000 bila kiasi cha dharura cha tani 14,000. Hata hivyo, alisema uwezo huo wa uzalishaji wa viwanda vya ndani ulitarajiwa kufikiwa pale tu panapokuwa na hali nzuri ya hewa na ufanisi mzuri wa viwanda’’
Changamoto zilizojitokeza
Waziri Hasunga alitaja changamoto ambazo zimekumba msimu wa uzalishaji sukari wa Mwaka 2019/2020 zikiwemo mvua nyingi kupita kiasi ambayo imepelekea uvunaji wa miwa kuwa mgumu, mlipuko wa magonjwa ya miwa kama vile viding’ata wa njano na uharibifu wa mitambo ya baadhi ya viwanda na kuchelewa kupatiwa vipuri.
Alisema sababu hizo zote kwa pamoja zimechangia kwa kiasi kikubwa Viwanda vyetu vya ndani kushindwa kufikia malengo ya kuzalisha tani 378,000 za sukari kwa msimu wa 2019/20.’’
Kauli ya Waziri Bashungwa
Waziri wa Viwanda na Biashara, Bashungwa alisema kutokana na hali halisi ya uzalishaji wa ndani wa sukari kuwa pungufu ya malengo ya uzalishaji, Serikali ilifanya makadirio ya kiasi cha sukari ya kuziba pengo la uzalishaji (gap sugar) na kutoa vibali kwa wazalishaji ili kuweza kuagiza na kuingiza sukari hiyo Nchini kwa wakati kwa ajili ya kukidhi mahitaji.
“Hadi hivi sasa tunazungumza na nyinyi, sukari iliyoagizwa kuja kuziba pengo la uzalishaji takribani tani 10,710 imeshaingia nchini na inaendelea kusambazwa katika mikoa yote,”alisema.
“Aprili 24, 28 na 30 Aprili, 2020 tunategemea kupokea jumla ya tani 13,500 za sukari ya kuziba pengo na tutaendelea kupokea kiasi kingine cha sukari mwanzoni mwa Mwezi Mei, 2020.
Kiasi chote cha sukari kilichopo nchini na tunachoendelea kupokea kinatosheleza kabisa mahitaji ya sukari nchini. Kwa taarifa hii, tuwaombe wananchi wote kuwa watulivu kwa sababu nchi yetu inayo sukari ya kutosha.’’ Alisema Serikali haitakubali kuona wafanyabiashara wanapandisha bei kiholela
“Tunapenda kuwatangazia wafanyabiashara wote nchini wenye tabia hizi za kupandisha bei kiholela waache mara moja kwani Serikali haipo tayari kuona wananchi wake wanaumia kwa manufaa ya watu wachache,”alisema Bashungwa na kusisitiza;
“Serikali itachukua hatua kali kwa mfanyabiashara yeyote ambaye atabainika kujinufaisha kwa kuuza sukari bei ya juu kulikoni bei ya kawaida ya soko.’’
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam