December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaanza ujenzi maghala ya kisasa ya kuhifadhi bidhaa za afya

Na ReubenKagaruki,Timesmajiraonline,Dodoma

SERIKALI kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imeanza ujenzi wa ujenzi wa maghala ya kisasa ya kuhifadhi bidhaa za afya katika Kanda ya Mtwara na Dodoma ili kukidhi upungufu uliojitokeza.

Hatua hiyo inatokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali kwenye ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya, ongezeko la fedha za ununuzi wa bidhaa za afya na uwekezaji kwenye vifaa tiba ambao umeongeza mahitaji ya miundombinu ya kuhifadhia bidhaa za afya.

Hayo yamesemwa wiki iliyopita na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dodoma waliokuwa kwenye ziara ya kutembelea na kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na MSD katika Kanda ya Iringa na Kanda ya Dodoma.

Amesema ujenzi huo ukikamilika utagharimu kiasi cha sh. bilioni 40. “Kwa sasa mradi umefikia asilimia 55 kwa ghala la Mtwara na asilimia 58 kwa ghala la Dodoma,” alisema Tukai.

Ameongeza kwamba kukamilika kwa ujenzi wa maghala kutasaidia kuimarisha uhifadhi wa bidhaa za afya kwenye viwango stahiki, kusogeza huduma karibu na vituo vya kutolea huduma za afya, kupunguza gharama za uhifadhi na kuimarisha utunzaji wa bidhaa za afya.

Kwa mujibu wa Tukai ujenzi huu wa maghala unatarajia kuongeza nafasi ya uhifadhi wa bidhaa za afya kwa mita za mraba 12,000 ambapo kwa ghala lililopo Dodoma mita za mraba 7,200 zitaongezeka na ghala la Mtwara kiasi cha mita za mraba 4,800 zitaongezeka hivyo kufanya ongezeko la uhifadhi kutoka mita za mraba 56,858.57 na kufikia mita za mraba 68,858.57.

Katika hatua nyingine, Tukai amesema Serikali imeweza kufanya maboresho ya kiutendaji kwa kuteua Bodi ya Wadhamini na kufanya mabadiliko ya Menejimenti.

Amesema maboresho hayo yameimarisha usimamizi wa ununuzi wa bidhaa za afya kwa kuimarisha ufuatiliaji wa mikataba, kuhakikisha uwepo wa mikataba ya muda mrefu, kuimarisha mifumo ya TEHAMA na kuimarisha utendaji.

Aidha, amesema Serikali kupitia Bohari ya Dawa imeendelea kuongeza ununuzi wa bidhaa za afya kutoka kwa wazalishaji wa ndani, ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/24, bidhaa za afya zenye thamani ya sh. bilioni 22.1 zilinunuliwa kutoka kiasi cha sh. bilioni 14.1 mwaka 2021/22 ikiwa ni ongezeko la asilimia 57.

“Dhamira hii itasaidia kuongeza uzalishaji na kuvutia wawekezaji ambapo matumizi ya fedha za kigeni yatapungua na ajira zitatengenezwa nchini.

Katika kufanikisha adhma ya Serikali ya kushirikisha sekta binafsi, alisema MSD imetambua maeneo yanayohitaji ushirikiano na sekta binafsi na inafanya uchambuzi ili wawekezaji wenye sifa waweze kushiriki kwenye uanzishaji wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za afya.