November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaanza kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi

Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online, Shinyanga

SERIKALI imeanza utekelezaji wa uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa baadhi ya vijiji wilayani Kishapu mkoani Shinyanga vilivyopitiwa na mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ili kuweka utaratibu mzuri wa matumizi ya ardhi katika vijiji hivyo.

Hali hiyo imelenga kuepusha matumizi holela ya ardhi katika vijiji hivyo kutokana na uwepo wa shughuli nyingi za kibinadamu zitakazofanyika baada ya reli hiyo kuanza kufanya kazi itakayoweza kusababisha baadhi ya miundombinu ya reli hiyo kuharibiwa.

Ofisa Mipango miji na vijiji kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi bora ya Ardhi, Fadhili Makame akizungumza na wanakijiji cha Mwigumbi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

Mtaalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi kutoka Dodoma, Ofisa Mipango Miji na Vijiji,Fadhili Makame amesema mpango wa matumizi bora ya ardhi utahusisha utengaji wa maeneo kwa ajili ya matumizi ya rafiki ya ardhi katika mradi huo hivyo kuilinda miundombinu ya reli.

Amesema mpango huo mbali ya kuhusisha utengaji wa maeneo kwa ajili ya matumizi ya ardhi ambayo ni rafiki kwa mradi vilevile utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua migogoro ya ardhi itakayokuwa ikijitokeza katika kijiji husika kutokana na kuundwa kwa kamati za vijiji zitakazokuwa zikisikiliza na kutatua migogoro hiyo.

“Kijiji cha Mwigumbi ni miongoni mwa vijiji ambavyo vitanufaika na mpango huu, tunaposema mpango wa matumizi bora ya ardhi tunamaanisha ni utaratibu wa kupendekeza namna mbalimbali ya matumizi ya ardhi kwa lengo la kuinua uchumi wa mwananchi, upimaji huu unafanyika bure hakuna mwananchi atakayetozwa fedha,”amesema Makame.

Pia amefafanua kuwa binadamu na mifugo ni vitu vinavyoongezeka kila siku lakini ardhi yenyewe haiongezeki,wakati Tanzania ikipata uhuru wake mwaka 1961 ilikuwa na watu wasiozidi milioni kumi lakini hivi sasa kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 idadi ya watanzania ni zaidi ya milioni 60.

Viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Mwigumbi wakiwa katika mkutano wa kuridhia utekelezaji wa mpango wa uandaaji matumizi bora ya ardhi katika kijiji chao, mwenye kofia ni Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji, Sospeter Mapinda.

“Kutokana na hali hiyo ni lazima pawe na utaratibu mzuri wa matumizi bora ya ardhi ili kusudi itumike ipasavyo na kuondoa migogoro ya ardhi maana pamoja ongezeko kubwa la binadamu na mifugo ardhi yenyewe haijaongezeka ni dhahiri kila mtu atagombania ili kupata ardhi,”ameeleza Makame.

Kwa upande wao wakazi wa kijiji cha Mwigumbi Kata ya Mondo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuwapatia fursa hiyo ambayo itawawezesha wao kumiliki ardhi inayotambulika kisheria na kwamba hatimiliki watakazopatiwa zitawasaidia kukopesheka kwenye taasisi za kifedha.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mwigumbi Sospeter Mapinda ameipongeza serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kitendo chake cha kuruhusu upimaji wa maeneo yao kufanyika bure na kwamba mpango huo sasa utaongeza thamani ya ardhi wanayoimiliki na utamaliza migogoro ya ya ardhi ya mara kwa mara.

Aidha Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwigumbi, Grace Fumbuka, mbali ya kuishukuru serikali kwa kukiteua kijiji chake kuwa miongoni mwa vijiji vitakavyotekelezewa uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi pia amesema kukamilika kwa mpango huo kutamaliza migogoro ya ardhi ambayo hujitokeza mara kwa mara kwenye kijiji hicho.

“Naishukuru serikali ya Rais Samia,nasema asante, hata wananchi wangu wameupokea mpango huu kwa furaha kubwa hasa pale walipoelezwa zoezi la upimaji litafanyika bure,kukamilika kwa mpango huu kutamaliza kabisa migogoro ya mara kwa mara ya kugombania ardhi hasa kati ya wakulima na wafugaji,”ameeleza Fumbuka.

Baadhi ya wanakijiji cha Mwigumbi Kata ya Mondo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wakiwa kwenye mkutano wa majadiliano kuhusu uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika kijiji chao.