Na Cresensia Kapinga, TimesMajira,Online Songea.
WANANCHI wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wameipongeza Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa Daraja la Mto Ruhuhu, kwani walikuwa wakiteseka kwa muda mrefu kuvuka mto huo wenye mamba na hata wakati mwingine ndugu zao walipoteza maisha wakivuka kwenda upande wa pili kutafuta mahitaji hasa huduma za afya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari jana wananchi wa Kijiji cha Kipingu Wilaya ya Ludewa na Lituhi Wilaya ya Nyasa, wamesema daraja hilo ambalo lina urefu wa mita 100 sawa na uwanja wa mpira wa miguu, litakuwa mkombozi wakati wa msimu wa masika ambapo maji yanakuwa mengi.
Mkazi wa Kipingu Ludewa, Erasims Mbeya amesema kukamilika kwa daraja hilo ambalo linaziunganisha Wilaya za Ludewa na Nyasa kutawaondolea kero na changamoto kubwa.
Amesema daraja hilo litawasaidia kuvuka upande wa pili na kuweza kununua mahitaji muhimu pamoja na kwenda kupata matibabu katika hospitali ya Lituhi na Peramiho ambazo ndizo zipo jirani tofauti na awali, ambapo walilazimika kulipa sh. 3,000 hadi 5,000 nyakati za masika ili kuvushwa na mtumbwi kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine .
Naye Malichuma Haule ameishukuru Serikali kwa jitihada ambazo imezifanya, kwani wanawake wajawazito walijifungulia njiani na wengine ndani ya maji wakati wakivushwa kwenda hospital.
“Naipongeza Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa daraja hili muhimu ndugu zetu wengi wamepoteza maisha kwa kuliwa na mamba au kusombwa na maji wakati wakivuka mto Ruhuhu , pia wajawazito walishindwa kuvuka na kujifungulia njiani, hivyo ujenzi wa daraja hili utasaidia wananchi kuondokana na mateso ambayo yalikuwa makubwa.
Tulipoteza mazao yetu kwa kusombwa na maji wakati tukiyavusha kwenda kuuza,”amesema Haule.
Aidha, aliwashukuru mafundi na wataalam waliokamilisha ujenzi wa daraja hilo ambalo litawanufaisha si wananchi peke yao, bali na Serikali itaongeza mapato kupitia daraja hilo pindi wakulima wanapopeleka kuuza mazao yao ya biashara.
Kwa upande wake mkazi wa Kipingu, Upendo Chale amesema wananchi walipitia mateso makubwa, kwani hata kivuko kilikuwa kikishindwa kuwavusha wananchi kutokana na maji kuwa machache nyakati za kiangazi, hivyo walilazimika kulipa sh 1,000 hadi 5,000 kuvuka kwa mitumbwi .
Meneja wa Tanroad Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Lazack Alinanuswe, amesema ujenzi wa daraja hilo ulianza Juni, mwaka 2016 ambapo kazi kubwa ilikuwa kujenga nguzo na misingi yake.
Amesema mkataba ulikamilika Septemba 2020 ambapo mfadhili alikuwa Serikari ambapo gharama ya mradi ni sh. Bilioni 6.1.
Aidha amewataka wananchi kulilinda daraja hilo na kwani vyuma vilivyotumika kujengea daraja ni vya gharama kubwa, hivyo hategemei kuona uharibifu wa aina yoyote.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu