Severin Blasio, TimesMajira Online, Morogoro
SERIKALI imeahidi kuendelea kutatua changamoto zinazoikabili Mamlaka ya Kudhibiti Manunuzi ya Umma (PPRA) zikiwemo kulipa madeni ya watumishi, watoa huduma na wazabuni ili kuiwezesha mamlaka hiyo kufanya kazi kwa ufanisi.
Pia serikali itaendelea kuhimiza kutumia mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Elektroniki (TANePS) kwa ajili ya mamlaka hiyo kuongeza ufanisi katika mchakato wa ununuzi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Michael John kwenye ufunguzi wa mkutano wa nne wa baraza la tatu la wafanyakazi wa PPRA lililokutana kujadili mipango ya bajeti iliyoidhinishwa mwaka wa fedha 2020/21 na changamoto zinazoikabili mamlaka hiyo.
“Wizara itaendelea kushirikiana na Menejimenti kuhakikisha changamoto zilizoainishwa zinatatuliwa kadri inavyowezekana…kuhusu upungufu wa watumishi, suala hili nalichukua na nitalifanyia kazi katika ngazi husika,” amesema John.
Pia ameitaka PPRA, kuhimiza taasisi za umma 540 kuhakikisha zinaunganishwa na mfumo wa TANePS ambao umedhihirisha kuwa mwarobaini wa changamoto ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwenye michakato ya ununuzi umma.
Awali Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Mhandisi Leonard Kapogo amesema, mamlaka inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi muhimu ya utawala bora, ikiwemo kuzielekeza na kuzisimamia taasisi nunuzi kufanya ununuzi kwa kuzingatia weledi, uadilifu, uzalendo, uwazi na kuheshimu miiko ya utumishi wa umma.
Mhandisi Kapogo amesema, hadi kufikia Juni mwaka huu taasisi 511 sawa na asilimia 94.7 ya taasisi za umma, zilikuwa zimeunganishwa na mfumo wa TANePS.
Ili kuhakikisha hayo yote yanatekelezeka, mamlaka imeandaa mchakato wa mapitio kwenye nyenzo za ununuzi na miongozo, sambamba na kuandaa nyaraka na mafunzo kuhusu sheria ya ununuzi wa umma na kanuni zake.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja