Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online Simiyu
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, kuchukua hatua mara moja kudhibiti viboko na tembo katika eneo la Kisesa, wanaohatarisha maisha na kurudisha nyuma shughuli za kiuchumi kwa wakazi hao.
Nchimbi ameyasema hayo Oktoba 7, 2024 kwenye mkutano na wananchi wa Jimbo la Kisesa Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, akiwa kwenye muendelezo wa ziara yake ya siku 7 katika Mkoa wa Simiyu na Shinyanga.
Amesema, Chama cha CCM kimejielekeza katika kushughulikia kero na changamoto za wananchi ikiwa pamoja na kuwapunguzia umasikini, hivyo ameitaka Serikali kushughulikia suala hilo kwa haraka ili wakazi wa maeneo hayo waendelee kufanya shughuli zao kwa amani.
“Kuhusu uvamizi wa tembo na viboko niiombe Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kuchukua hatua mara moja kudhibiti hao tembo na viboko wanaofanywa uharibifu wa makazi ya watu na mazao, CCM inaelekeza katika kupunguza umasikini kwa wananchi na suala la wanyama hao waharibifi wanarudisha nyuma shughuli zao za kiuchumi hivyo ni vyema mkadhibiti mara moja” amesema Nchimbi.
Pia, akizungumzia suala la stakabadhi ghalani, Nchimbi amesema ni sera ya CCM baada ya utafiti wa kina uliofanywa na wataalamu mbalimbali katika nchi na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025.
“Tunapozungumzia suala la stakabadhi ghalani ni utafiti uliofanywa na wataalamu ambapo pia ni mkataba kati ya wananchi na CCM, ambapo kiongozi au mgombea akichaguliwa anaenda kuwaeleza wananchi kuwa tutatekeleza sera ya stakabadhi ghalani hivyo hiyo ni sera ya CCM inayoeleweka”, ameongeza Nchimbi.
Ameeleza kuwa, hatua hiyo ilifuata baada ya wafanyabiashara wakubwa kufanya vikao na kupanga bei kubwa zinazoumiza wananchi ” wananchi kwa maelfu walikuwa wanaumia kwa bei kwani Kuna vitu vingine vilikuwa vinauzwa bei tofauti na ilivyo Sasa uwongo ukweli? kwa hiyo hali ipo poa sasa lakini CCM sio Chama mfu ni Chama ambacho kinaenda kutazama hali kila siku.
Aidha kwa upande wake, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA Amos Makalla, ameendelea kuwaomba wananchi kuendelea kukiamini CCM na kudai kuwa, chama hicho ndicho chenye dhamana ya kuwaletea maendeleo wananchi ikiwa pamoja na kutatua kero zao.
Katika ziara hiyo Nchimbi ameambatana na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA Amos Makalla na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdallah Hamid.
More Stories
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania