Na Mwandishi wetu, Timesmajira online
Serikali ya Ujerumani imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika hatua zake za kukuza na kuendeleza shughuli za Uhifadhi kupitia miradi mbalimbali ambayo nchi hiyo inafadhili katika sekta ya wanyamapori
Hayo yamebainishwa leo Jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Selemani Mkomi, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini Dkt. Katrin Bornemann.
Amesema Serikali ya Ujerumani ni miongoni mwa wadau wakubwa wa shuguli za Uhifadhi hapa nchini na wamekuwa wakifadhili miradi mbalimbali ya Uhifadhi inayosaidia kuleta ustawi wa wanyamapori.
“Serikali ya Ujerumani imeahidi kwamba itaendelea kushirikiana na Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya wanyamapori hususan ujangili na mabadiliko ya tabia nchi ” amesema Naibu Katibu Mkuu Mkomi.
Amesema licha ya Serikali ya Ujerumani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kuweza kufadhili miradi mbalimbali ya uhifadhi kwa kutoa kiasi cha jumla ya shilingi milioni 350 imesema itashirikiana zaidi na Tanzania katika kuhakikisha maisha ya wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya Hifadhi yanaendelea kuboreka
Kwa upande wake Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini Dkt. Katrin Bornemann amesema kuwa nchi yake imeridhishwa na utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na nchi yake ikiwemo vita dhidi ya ujangili
Kufuatia hali hiyo Dkt.Katrin amesema kuwa nchi yake itaendelea kusaidia shughuli za uhifadhi ikiwemo Mpango wa Usimamizi wa migogoro kati ya Binadamu na Wanyamapori ili kuzipunguzia umasikini Jamii za Watanzania wanaoishi karibu na maeneo ya Hifadhi
“Moja ya shabaha yetu kama nchi wahisani ni kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya Hifadhi hawaathiriwi na wanyamapori wakali na waharibifu” amesisitiza Dkt.Katrin
Kwa sasa miradi inayoendelea iliyofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani katika sekta ya Uhifadhi ni mfumo wa Ikolojia wa Serengeti, Selous na Mfumo wa Ikolojia wa Katavi-Mahale.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi