Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online
SEKTA ya Ujenzi ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi nchini, hii ni kutokana na miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji, Angellah Kairuki, pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa wamefanya kikao cha pamoja na wazalishaji wa saruji nchini kwa lengo la kujadili fursa mbalimbali, changamoto na namna bora ya kukuza sekta ya ujenzi nchini kupitia saruji, kikao kilichofanyika Ofisi za Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, mawaziri hao walikutana na kampuni tisa za saruji zikiwemo Dangote Cement.
Camel Cement, Nyati Cement, Mbeya Cement, Kilimanjaro Cement, Maweni Cement, Tanga Cement, Lake Cement, Twiga Cement pamoja na Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI), wakijadili namna bora ya kuendeleza sekta hiyo.
Waziri Bashungwa amewapongeza wazalishaji hao kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwasihi wasipandishe bei ya saruji kiholela hasa kuzingatia kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya tano ni kuiona Tanzania inakua nchi ya viwanda.
Wazalishaji hao walizungumzia changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo ikiwemo ubovu wa barabara hasa kipindi cha mvua, unaofanya bei kuwa juu kidogo, upatikanaji wa nishati madhubuti kama gesi, suala la kodi na kuiomba serikali sikivu kushughulikia changamoto hizo.
Naye, Waziri Kairuki amesema kuwa wizara yake na Wizara ya Viwanda wanafanya kazi kwa ukaribu na kuwatoa hofu wazalishaji hao wa saruji kuwa Serikali ipo pamoja nao na inashughulikia changamoto zao na kuwahakikishia wizara yake yenye dhamana ya uwekezaji itahakikisha inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji hao.
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Bashungwa aliwahakikishia wazalishaji hao kuwa serikali ina angalia namna bora ya kuhakikisha gesi inapatikana kwa urahisi hasa kwa viwanda vilivyopo Ukanda wa Pwani pia amewahakikishia kuwa changamoto nyingine ndogo ndogo atazishughulikia ndani ya wiki moja ijayo.
More Stories
Samia apeleka neema Tabora, aidhinisha Bil. 19/- za umeme
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka
TARURA yaomba Mkandarasi aitwe