December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali, wadau kushirikiana kufanikisha mageuzi ya Elimu

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema Sekta ya Elimu ipo kwenye mageuzi makubwa ya elimu na hivyo kuhitaji wadau wengi kushirikiana na Serikali katika kufanikisha mageuzi hayo.

Prof. Nombo amesema hayo jijini Dodoma alipokutana na wawakilishi kutoka Benki ya Stanbic waliofika ofisi kwake kwa lengo la kutambulisha programu na bidhaa za benki zinazochangia maendeleo ya Sekta ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kuona namna ya kushirikiana katika utekelezaji wenye tija.

Amesema mwelekeo wa nchi kwa sasa ni kutoa elimu ujuzi ili kuzalisha nguvu kazi itayoweza kujiajiari na kuchangia katika maendeleo ya nchi.

“ Nimefurahi sana kuwa tunazungumza lugha moja na wadau , jana tulikuwa na Benki moja ya hapa nchini na imesema inatoa mafunzo kwa vijana 5000 inatia moyo maana huu ndio mwelekeo wa nchi, sasa kupitia programu yenu ya uwekezaji kijamii (CSI) mnaweza kuona tutashirikiana vipi katika eneo hili na lile la kukuza ubunifu. Nashauri pia mkutane na OR- TAMISEMI ambao ni wamiliki na waendeshaji wa shule,” amesema Prof. Nombo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. James Mdoe amewaomba kuangalia maeneo ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa lengo la kuwaendeleza wabunifu wazawa lakini pia kusaidia wanafunzi wa vyuo vya kati na vyuo vikuu kupata elimu ya fedha.

Akizungumza katika kikao hicho Meneja Mawasiliano wa Benki ya Stanbic Doreen Diminic amesema lengo la kuwa na kikao na Wizara ni kuona maeneo ya kipaumbele ambayo Benki inaweza kushirikiana na Wizara pamoja na wadau wengine katika kuhakikisha elimu ya mtoto wa kitanzania inakuwa bora.

Amesema tangu benki hiyo kuanza mwaka 1995 imekuwa pamoja na kufanya shughuli za kibishara lakini kurejesha kwenye jamii kile wanachozalisha ikiwemo kununua madawati na kujenga miundombinu ya shule lakini pia kwa sasa benki mekuja na program ya National School Championship kwa ajili ya kutoa elimu ya ujasiriamali na fedha kwa wanafunzi.

“Mahali pote tulipo tunafocus kwenye elimu ndio kipaumbele cha Benki na ndio maana leo tumefika hapa Wizarani kuona namna tunavyoweza kushirikana, tunashukuru tumepata mwelekeo sahihi wa maeneo ya kuchangia,” amesema Doreen.