March 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuzindua Sera ya Ardhi ya 1995 Toleo la 2023

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

SERIKALI inatarajia kuzindua Sera ya Ardhi ya Mwaka 1995 ,Toleo la 2023 iliyolenga kuongeza ufanisi katika sekta ya ardhi kwa ujumla

Akizungumza Machi 15 mwaka huu na waandishi wa habari Jijini Dodoma,Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius  Ndejembi amesema uzinduzi huo utafanyika Machi 17 mwaka huu katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete. 

“Sera hii inalenga kuimarisha usimamizi wa ardhi kwa kuongeza ufanisi wa utawala, kutatua migogoro ya ardhi, na kuweka mifumo inayosomana ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na ufuatiliaji wa shughuli za ardhi.”alisema Ndejembi na kuongeza kuwa 

“Sera hii itaongeza uwazi na ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya ardhi, kuwezesha uwekezaji endelevu, na kulinda haki za wamiliki wa ardhi vijijini na mijini.”

Ndejembi alisema,uzinduzi huo utahudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo mabalozi wanaowakilisha Nchi zao hapa nchini  pamoja na Wadau wa ardhi

Aidha alisema Sera hiyo itazinduliwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan huku akisema kaulimbiu  ya uzinduzi huo ni “Sera ya Ardhi Msingi wa Ustawi na Malengo Endelevu ya Taifa”