Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
SERIKALI imeanza mchakato wa maandalizi ya Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo itatoa maono na kuweka malengo ya miaka 25 ijayo lakini pia kukidhi matakwa ya Katiba ya nchi ambayo ndiyo mwongozo wa nchi.
Akizungumza leo Machi 30,2023 na waandishi wa habari jijini Dodoma,Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Jenifa Omolo amesema  uzinduzi wa Dira hiyo inatarajiwa kufanyika April 3, 2023 jijini Dodoma  huku akiwaasa wadau wote kushiriki kikamilifu kutoka katika maeneo yao.
 “Maandalizi ya Dira mpya ya 2050 yanakidhi matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndio mwongozo mkuu wa nchi yetu. “amesema Omolon kuongeza kuwa
“Historia ya upangaji wa mipango nchini imeanza kuanzia nchi ilivyopata uhuru ambapo matamanio yalikuwa juu ya kupambana na ujinga, umaskini na maradhi ambapo katika kuhakikisha azma hii inafikiwa, kuliandaliwa mipango ya vipindi tofauti tofauti. “
Amesema,mnamo 1964, Tanzania ilifanikiwa kuandaa Mpango wa kwanza wa Muda mrefu wa miaka 15 ambao ndani ya utekelezaji wake uliimarishwa na Azimio la Arusha la mwaka 1967.
Kwa mujibu wa Niabu Katibu Mkuu huyo,Mpango wa Pili wa Muda mrefu uliandaliwa Mwaka 1981 ambao ulipangwa kutekelezwa kupitia mipango minne ya miaka mitano na kwamba utekelezaji wa mipango hiyo ulienda sambamba na utekelezaji wa programu mbalimbali zilizosimamiwa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia (WB) zilizokuwa na lengo la kuleta utulivu wa kiuchumi na marekebisho ya kimuundo chini.
Vile vile amesema,Serikali ilianza mchakato wa maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa (TDV 2025) mwaka 1995 ambao ulikamilika mwaka 2000 na kwamba utekelezaji wa Dira hii ulianza kupitia programu za kupunguza umaskini ambapo programu ya kwanza ilikuwa ni Mkakati wa Kupunguza Umaskini (PRS I) mwaka 1999/2000 hadi 2002/03.
“Mkakati wa pili kutoka 2004/05 hadi 2009/10 ambao pia unajulikana kama Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA I), na Mkakati wa tatu ulitelezwa kuanzia mwaka 2010/11 hadi 2014/15, ambao ulijulikana kama MKUKUTA II. “
Kwa mujibu wa Omolo katika mwaka 2009/10, Serikali ilifanya tathmini ya utekelezaji wa Dira 2025 kupitia mikakati na programu za maendeleo huku akisema kuwa tathmini hiyo ilibainisha uhitaji wa Taifa kuanza kupanga vibaumbele vya nchi.
“Suala hili lilipelekea kuandaliwa kwa Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu (LTPP) 2011/12 – 2025/26),Mpango huu wa miaka 15 ulipangwa kutekelezwa kwa mipango ya muda wa kati ya miaka mitano mitano mitano na mipango ya muda mfupi ya mwaka mmoja . “amesisitiza
Amesema,katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025, Taifa limeweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo katika nyanja mbalimbali hususan za kijamii, kiuchumi na kisiasa na kwamba utekelezaji wa Dira 2025 unafikia tamati mwaka 2025.
“Kwa msingi huo , ni jukumu letu sote kwa nafasi zetu kuanza kufikiria juu ya mafanikio ya utekelezaji wa dira 2025 na mustakabali wa nchi yetu katika miaka ya mbele ijayo. Taja mafanikio hapa ya TDV 2025 .
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba