November 9, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuwezesha CBE kuwa kituo mahiri

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

SERIKALI imeahidi kuendelea kukiwezesha Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), ili kiwe kituo Bora cha umahiri kwa nchi za Afrika Mashariki,Kati na Kusini mwa Afrika.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar- es -Salaam na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, wakati wa mahafali ya 59 ya CBE, ambapo wahitimu 2,665 walitunukiwa vyeti katika ngazi mbalimbali.

Amesema, Serikali inajivunia chuo hicho,ambacho kimekuwa mahiri kwa kutoa wanataaluma wanaotegemwa kwenye viwanda na kampuni mbalimbali, ndani na nje ya nchi.

“Ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na chuo hiki,ni ishara kuwa nikimbilio kwa wananchi wengi, tutaendeleza ubora wa elimu inayotolewa hapa.Tunataka iwe elimu ya vitendo iwawezeshe wahitimu kuajiriwa na kujiajiri,”amesema.

Pia amesema,Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya chuo hicho,yakiwemo majengo ya mihadhara na madarasa ili kuongeza kiwango cha wanafunzi wanaodahiliwa kila mwaka.

Kigahe ameaema,maboresho yote yatafanyika kwenye kampasi zote za chuo hicho ambazo ziko kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Dodoma.

Hata hivyo,Serikali inaagiza tafiti mbalimbali zinazofanywa na CBE,ziende kuwasaidia wajasiriamali.Kwani inaonekana vijana wengi hawana uthubutu wa kufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali.

Mkuu wa chuo cha CBE, Profesa Edda Lwoga, amesema chuo hicho kimekuwa na mafanikio tangu kuanzishwa mwaka 1965 ,kwa kuwa na wahitimu wengi ambao wako serikalini na sekta binafsi.

Amesema,CBE inajivunia kuzalisha idadi kubwa ya wataalamu wa biashara ambao wamekuwa wakitoa mchango mkubwa kwenye uchumi.

Hata hivyo, amesema chuo hicho,kimetekeleza majuku yake ya msingi kama kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu kwenye sekta ya biashara, metrolojia na viwanda.

“Tulianza na wanafunzi wachache,lakini sasa tuna wanafunzi zaidi ya 20,000 kwenye kampasi zetu nne,Dodoma, Mwanza na nyingine Mbeya,”amesema

Aidha amesema,mitaala ya chuo hicho pia imejikita kwenye sekta ya utalii, ununuzi na ugavi,tehama, vipimo na viwango.Ni chuo pekee kinachotoa elimu ya vipimo na viwango kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.

“ Katika kusogeza huduma yetu ya elimu ili iweze kufika maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi,tulianza kutoa shahada za uzamili kwa njia ya mtandao na zimepokelewa vizuri na wananchi na mpaka sasa tumetoa shahada nane,” amesema Profesa Lwoga.

Alisema wanatoa Shahada za Uzamili kwenye eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), usimamizi wa miradi na biashara za kimataifa usimamizi wa fedha na biashara.

“Katika kuboresha mitaala yetu mwaka 2021 tulizindua mwongozo wa atamizi za biashara ambapo wanafunzi wanasajili bunifu zao za biashara,tunawaendeleza wanafanya baishara wakiwa chuoni mpaka sasa vijana zaidi ya 412 wanaendelea na biashara kupitia mfumo huo,”.