December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuweka ukomo matumizi ya kuni,mkaa

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema,amezisisitiza wizara na taasisi zinazopika chakula cha pamoja cha kuanzia watu 10 kuendelea ,kutumia nishati safi ya kupikia katika mapishi ya vyakula wanavyotumia huku akisema sasa serikali imeanza kuhamasisha mtu mmoja mmoja kutumia nishati safi ya kupikia badala ya mkaa na kuni.

Aidha amesema,hapo siku za mbele ,Serikali itaweka ukomo wa matumizi ya mkaa na kuni huku akisisitiza kila mmoja aanze kubadilika sasa kuachana na matumizi ya mkaa na kuni na badala yake aanze kutumia nishati safi ya kupikia.

Akifunga Mkutano wa Maalum wa Viongozi na wadau wa mazingira ulioitishwa ili kujadili mwenendo wa wa mazingira nchini,Majaliwa amesema,hatua hiyo inalenga kulinda mazingira hapa nchini.

“Tayari tumeshaanza kutoa miongozo ,tumeanza na taasisi kuanzia watu 10 wanaopikiwa chakula cha pamoja ambapo sasa chakula hicho kitapikwa kwa gesi au umeme,

“Na tumezitaka Wizara zake zifanye hivyo ,lakini pia sasa tumeanza na mtu mmoja mmoja.”

Amesema Serikali imetoa fursa kwa wajasiriamali kuanzisha biashara ya kuuza mitungi na majiko ya gesi hadi kwenye ngazi ya vijiji ili nishati hiyo iweze kupatikana kwa urahisi.

 “Rais wetu amekuwa kinara wa nishati safi ,na mwezi Mei alienda Ufaransa kuhutubia kuhusu nishati safi na yeye akiwa ni Mwenyekiti mwenza wa mkutano huo,hii ni fahari kwa nchi yetu,na sisi wananchi tumuunge mkono” amesisitiza

Katika kukabiliana na changamoto za uchafuzi wa mazingira, Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua hatua za kisera na kimkakati ili kuleta matokeo chanya.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi (OMR – Muungano na Mazingira), Dkt. Ashatu Kijaji amesema mkutano huo maalum ulihudhuriwa na washiriki 2,500 kutoka maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Zanzibar.