Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WAZIRI wa Kilimo na Umwagiliaji Hussein Bashe amefurahishwa na juhudi zinazofanywa na mashirika yanayojihusisha na utoaji huduma za bima ya mazao kwa wakulima na kuahidi kuwapa ushirikiano ili kufanikisha malengo yao.wanu kuhakikisha majanga ya asili yanadhibitiwa kikamilifu.
Ametoa kauli hiyo alipokuwa akizindua Muunganiko wa Mashirika ya Bima (Konsotia) jana katika viwanja vya Ipuli Mkoani hapa.
Alisema muunganiko huo ni muhimu kwa kuwa utasaidia kutatua baadhi ya changamoto zilizopo na kuahidi kuwa serikali itaendelea kuwawekea mazingira wezeshi ili kufanikisha malengo yao.
Aidha aliutaka muunganiko huo kupanua wigo wa huduma zake kwa kuhakikisha majanga yote yanayowakumba wakulima yanapata ufumbuzi hasa mabadiliko ya bei wakati wa masoko.
‘Hii ni hatua nzuri ya kuboreshwa kwa huduma za wakulima ikiwemo kutatua changamoto zao hasa wanapopata majanga kama ukame na mvua za mawe, lakini pia muangalie na mabadiliko ya bei katika masoko,’ alisema.
Kwa upande wa Kamishina wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) Dkt. Baghayo Saqware alieleza kuwa muunganiko huo utasaidia wakulima wengi pindi majanga yatakapotokea. Alisema wamekusanya mtaji wa kutosha kutoka kwenye mashirika mbalimbali ili kuwafikia wakulima nchini kote.
Mtendaji wa Umoja wa Mashirika hayo Elia Kajiba alimhakikishia Waziri kuwa gharama za kulipia bima ya mazao zitaangalia vigezo maalumu kulingana na ukubwa wa mashamba na mapato ya mkulima.
Aliongeza kuwa mamia ya wakulima wamepata elimu ya bima ya mazao kupitia muungano huo ambao umezionduliwa rasmi katika maadhimisho hayo ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) .
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja