November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kusaidia wanawake wenye ulemavu

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imejidhatiti katika kuhakikisha inasaidia Wanawake hasa wenye ulemavu kupata fursa mbalimbali za kujikwamua kiuchumi hasa kupata mikopo kwaajili ya mitaji ya shughuli za kiuchumi.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wakili Amon Mpanju alipokutana na kuzungumza na uongozi wa Shirikisho la Vyama vya walemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Jijini Dodoma.

“Tuna Idara ya Maendeleo ya Jinsia hapa Wizarani, Mkurugenzi husika hakikisha mnaandaa mkutano wa wanawake wenye ulemavu nchini kujua changamoto zinazowakabili katika masuala ya mikopo na uwezeshaji wa kiuchumi” alisema Wakili Mpanju

Aidha Wakili Mpanju ametumia fursa hiyo kulipongeza shirikisho la Mabenki nchini kwa namna wanavyozidi kuboresha miundombinu ya Mabenki na baadhi ya mifumo ambayo imekua msaada kwa watu wenye walemavu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirikisho la Watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA) Jonas Lubago ameiomba Serikali kuboresha utoaji wa mikopo hasa ile ya asilimia 10 ( 2% kwa watu wenye ulemavu) inayotolewa na Mamlaka ya Mikoa na Serikali za Mitaa ili iweze kuwafaisha watu wenye ulemavu.

Pia Luboga ameishukuru Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi kwa ushirikiano wanaopata kupitia wataalam mbalimbali katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashiriki katika shughuli za kijamii na hasa za kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Jinsia, Rennie Gondwe na Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii Tullo Masanja kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na baadhi ya wajumbe kutoka Shirikisho la watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA) nchini.