October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kupunguza gharama za uendeshaji sekta ya utangazaji kwa asilimia 40

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

SERIKAILI kupunguza gharama za uendeshaji wa sekta ya utangazaji kwa kurekebisha viwango vya ada za leseni kwa takribani asilimia 40 pamoja na kusimamia zaidi sekta hiyo.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Februari 13,2023 na Naibu Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa watoa huduma wa sekta ya utangazaji ikiwa pia ni maadhimisho ya siku ya radio Duniani kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Nape Nnauye.

Mha.Kundo amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya ukuzaji wa sekta ya utangazaji nchini kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambapo hatua ya kwanza Serikali kuchukua ni kupunguza ada za mwaka za leseni za utangazaji .

Pia ametaja maboresho mengine yanayofanywa katika sekta ya habari nchini ni pamoja na kuanzishwa kwa sheria ya ulinzi wa Taarifa binafsi ya mwaka 2022(Data  Protection Act ,2022) inalenga sekta ya utangazaji nchini.

“Kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia ni kuhakikisha watoa huduma za utangazaji hasa radio zinazidi kuwa na tija katika uchumi wa vituo na taifa kwa ujumla”amesema.

Kwa upande wake  Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabir Bakari, amesema kuwa  vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi kidijiti kwa kuwa matangazo mengi yamehamia kwenye njia hiyo.

Dkt.Jabir ametaja idadi ya watoa huduma za habari nchini ambapo amesema kuna jumla ya watoa huduma wapatao 787.

“Mkutano huu umeandaliwa kwa lengo la kutafakari mchango wa sekta ya utangazaji katika jamii kwani vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuchangia kukuza uchumi wa kidijiti nchini,

“Mkutano huu utajadili changamoto zinazoikabili sekta ya utangazaji pamoja na hali ya sasa ya sekta hii na kutoa maazimio pia mkutano huu umekwenda sambamba na maandalizi ya maonyesho ya vifaa mbalimbali vya utangazaji yatakayofanyika hapa”amesema.