January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani 

Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza

Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF), imeanza kupeleka huduma ya  mawasiliano kwenye maeneo ya mipakani,ili kutatua changamoto ya muingiliano wa mawasiliano baina ya wakazi wa maeneo hayo na wa nchi jirani.

Hayo yameelezwa Januari 21,2025 jijini Mwanza na Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA)Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali, wakati wa semina kwa Wahariri, waandishi na watangazaji wa vyombo vya habari, kuhusu taarifa za mwenendo wa sekta ya mawasiliano kwa robo ya pili ya mwaka wa 2024/2025 (Oktoba hadi Desemba 2024).

Mhadisi Imelda,amekiri kuwa siyo maeneo yote ya mipakani ambayo ya yamefikiwa  na huduma ya mawasilianoHivyo Serikali imeweka jitihada kupitia UCSAF,kuhakikisha  maeneo ya mipakani  yanafikiwa na huduma hiyo, kuboresha usikivu wa redio ili wakazi wa maeneo hayo wapate taarifa ya mambo yanayoendelea  nchini na nje ya nchi.

“Serikali imekusudia kufikisha huduma ya mawasiliano kwa wananchi,si  kwa ajili kuwasiliana tu,pia kwa  kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi, mfano kama mtu ameona kitu ambacho ni hatari kwa usalama wa nchi, atatoaje taarifa na kufikisha kwa mamlaka bila kuwa na mawasiliano?, na jitihada hizi ni endelevu,”amesema  Mhandisi Imelda.

Awali akitoa ripoti ya Sekta ya mawasiliano kwa kipindi cha  Oktoba hadi Desemba,2024, Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta wa TCRA, Mhandisi Mwesigwa Felician,amesema sekta ya mawasiliano inazidi kukua, ambapo kwa Septemba mwaka 2024 laini za simu zilikuwa milioni 80.7, na hadi kufika Desemba,2024 ziliongezeka kwa asilimia 7.7 na kufikia laini milioni 86.8.

Mhadisi Felician,amesema ongezeko hilo pia limeenda kwa watumiaji wa huduma ya inteneti kutoka milioni 40 hadi kufikia milioni 48.0, huku watumiaji wa simu janja wakifikia milioni 23 na  matumizi ya intaneti yakifikia 617 PB.

Amesema kwa upande wa vifurushi , bei zinazidi kushuka ukilinganisha na bei ambazo zipo nje ya vifurushi,huku bei ya kupiga simu ndani ya nchi za Afrika Mashariki ikipungua tofauti na mtu anayepiga kutoka nchi nyingine kwenda nchi iliopo ndani ya Afrika Mashariki.

Mmoja wa washiriki wa semina hiyo Neema Emmanuel, amesema ripoti hiyo ya robo ya pili ya mwaka 2024/25,iliyowasilishwa imewafumbua macho na kuongeza uelewa juu ya mwenendo wa sekta ya mawasiliano nchini.