June 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kununua rani 200,000 za mbolea kulinda viwanda vya ndani

Na Joyce Kasiki Dodoma

SERIKALI imepanga kununua tani 200,000 za mbolea pamoja na tani 50,000 za chokaa kutoka kwa wazalishaji wa ndani kwa ajili ya matumizi ya kilimo.Waziri wa Kilimo,Hussein Bashe, amesema Serikali imeamua kuchukua hatua hiyo mahsusi kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani vinavyoanza kuimarika, huku ikiendelea kulinda mfumo wa ruzuku kwa wakulima.

Akizungumza jana jijini Dodoma, Waziri Bashe alisema ununuzi huo hautahusisha maeneo yenye matumizi makubwa ya mbolea, bali utalenga maeneo ambayo bado matumizi ya mbolea ni madogo, ili wakulima wapate fursa ya kuzielewa na kuona matokeo chanya ya mbolea zinazozalishwa ndani ya nchi.

Amesisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza matumizi ya mbolea kwa maeneo yaliyokuwa nyuma na hivyo kuongeza uzalishaji wa kilimo kwa kutumia bidhaa bora zinazotengenezwa na wazalishaji wa ndani.

Aidha, amebainisha kuwa mpango huo hautavuruga mfumo wa ruzuku uliopo, bali utakuwa wa kuunga mkono jitihada za kuwafikia wakulima zaidi.

Katika taarifa hiyo hiyo, Waziri Bashe ametangaza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kiwanda kipya cha mbolea cha Itracom Fertilisers Limited utakaoanyika Juni 28, 2025 hapa jijini Dodoma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Nduwimana Nazaire, amesema hadi sasa kiwanda kina uwezo wa kuzalisha aina 14 za mbolea zinazotengenezwa kwa kushirikiana na taasisi za serikali zikiwemo TARI na TFRA.

Ameeleza kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kutengeneza mbolea kulingana na mahitaji ya eneo, aina ya zao na mazingira ya kilimo.

Ameongeza kuwa mbolea zinazozalishwa ni mchanganyiko wa chumvi mbalimbali na malighafi za asili kama vile samadi, ili kutoa lishe kamili kwa mimea kulingana na mahitaji ya wakulima wa Tanzania.

Kiwanda cha Itracom Fertilisers Limited ni matokeo ya uwekezaji ulioanza miaka mitatu na nusu iliyopita na sasa kinatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mapinduzi ya kilimo nchini kupitia uzalishaji wa bidhaa bora za mbolea kutoka hapa hapa nchini.