Na Mbaraka Kambona,TimesMajira Online,Liwale
NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema katika bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali itajenga bwawa la kunyweshea Mifugo lenye thamani ya Shilingi Milioni 480 katika Kijiji cha Kimambi, Wilayani Liwale, Mkoani Lindi.
Ulega ameyasema hayo juzialipofanya ziara katika Wilaya ya Liwale, Mkoani Lindi kwa lengo la kusikiliza kero za Wafugaji na Wakulima ili kuzitatua.
Amesema ujenzi wa bwawa hilo utasaidia kutatua changamoto ya maji ambayo inawakabili wafugaji wa maeneo hayo na utasaidia pia kutatua migogoro baina yao na wakulima Wilayani humo.
“Rais Samia Suluhu Hassan anakwenda kuwajengea bwawa lenye thamani ya Shilingi Milioni 480 hapa Kimambi, ujenzi wa bwawa hilo utasaidia kuwaondosha katika migogoro,” amesema Ulega.
Naibu Waziri Ulega alisisitiza kuwa pesa hizo zipelekwe kufanya kazi iliyopangiwa ya ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo huku akiwataka viongozi wa Wilaya hiyo kuhakikisha pesa hizo zinatumika vizuri.
Aidha, amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amewapa pia Majosho mawili katika Kijiji cha Kimambi na Kijiji cha Luwele.
“Sasa kwa sababu huku mifugo imekuwa mingi sana, Mimi nakuongezeeni Josho lingine hapa ili mifugo mingi iweze kuogeshwa ,”ameongeza Ulega
Naye, Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea pesa hizo huku akisema kuwa bwawa hilo likikamilika hawatarajii tena kuona migogoro katika Vijiji vilivyotengwa kwa ajili ya Wafugaji Wilayani humo.
More Stories
CCM inabebwa na kazi nzuri za Rais Dkt. Samia-Makalla
Wananchi Babati wamshukuru Rais Samia kwa kuwafungulia barabara
Rais Samia aungwe mkono ajenda ya nishati safi ya kupikia