Serikali kuimarisha mikakati ya kukabiliana na maafa
Na Mwandishi Wetu,Dodoma
SERIKALI imesema inaendelea kuweka mikakati madhubuti namna ya kujikinga na kukabiliana na maafa ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kujitokeza na kuhatarisha usalama wa raia pamoja na kuharibu miundo mbinu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Balozi. Dkt Pindi Chana katika semina kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu dhana na Mfumo wa Usimamizi wa Maafa Nchini iliyoandaliwa na Idara ya Menejimenti ya Maafa katika Ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma.
“Hivi sasa Mheshimiwa Mwenyekiti nikuhakikishie elimu inayotolewa katika shule zetu za Msingi Sekondari na ngazi ya vyuo vikuu inalenga vijana wetu na jamii yetu kujua Maafa kwa ujumla ili kujikinga wasipate madhara,” alisema Mhe. Pindi.
Aidha alibainisha kwamba utafiti unaofanywa na watalaamu mbalimbali kuhusu Mazingira na Maafa utumike vyema kama moja ya njia ya kukabili maafa ya asili na yale yatokanayo na shughuli za kibinadamu. Utafiti hutoa mwanya wa kujua hatua sahihi za kuchukua kabla ya majanga kutokea na baada ya kutokea.
Wakti huo huo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bwn. Kaspar Mmuya alifafanua kwamba muswada wa sheria ya Maafa utasaidia kuondoa changamoto zilizobainika kutokana na sheria ya zamani na wahusika kufahamu majukumu yao ili kuepusha muingiliano wa majukumu wakati wa utekelezaji wa shughuli zote za Maafa.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Najma Giga alishauri Mfuko wa Maafa kutengewa bajeti yake itakayosaidia kutatua changamoto zinazotokana na Maafa badala ya kusubiri hadi yatokee na kuanza kutafuta wadau kwa ajili ya kutoa huduma.
“Tunaelewa waziwazi kuna Maafa ya kimaumbile ambayo huwenda yakatokea kila mwaka kutokana na mvua za masika au mabadiliko ya tabianchi kwenye fukwe zetu za bahari tunajua kabisa kila mwaka mabadiliko ya tabia nchi yanapotokea shemu ya ardhi inaliwa lakini ikitokea Maafa ndio tunaanza kupambana kutafuta wadau. Mfuko unaanza kutuna kwanini sasa serikali isione utaratibu utakaowekwa maalumu kwa hao hao watu wanaotusaidia,” alieleza Makamu Mwenyekiti huyo.
Akihitimisha wasilisho la dhana na Mfumo wa Usimamizi wa Maafa katika semina hiyo Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Charles Msangi alisema Muswada wa sheria imezingatia uwajibikaji wa wadau wote kwani ulifanyika utafiti ambao uliangalia majukumu ya kila mdau .
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam