Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepiga hatua kubwa kwa kuweka mifumo, sera na mikakati madhubuti ya kuzuia, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali ya pindi baada ya maafa yanapotokea, ili kuimarisha usalama na ustawi wa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu,Dkt. Jim Yonazi, wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya wakufunzi kuhusu usimamizi wa hatari zitokanazo na maafa Mafunzo hayo yaliandaliwa na Jumuiya ya Nchi Zilizopo kwenye Mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Uturuki (TİKA), Shirika la Msalaba Mwekundu la Uturuki, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania.



Dkt. Yonazi amesema kuwa mafunzo hayo yamekusudia kuimarisha uwezo wa kitaifa na wa kikanda katika kudhibiti maafa na kuwalinda wananchi. Alibainisha kuwa mafunzo hayo yanaonesha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kupunguza hatari za maafa (DRR), sambamba na kujenga jamii imara na endelevu.
“Kuwajengea uwezo viongozi wa jamii ni jambo la msingi, kwani wao ndiyo wahusika wa kwanza kutoa mwitikio wakati wa majanga, kusaidia kuratibu misaada na kuhakikisha usalama na ustawi wa jamii,” amesisitiza Dkt. Yonazi.
Aidha, amewapongeza wadau wote waliowezesha mafunzo hayo kufanyika kwa mafanikio, akiwemo TİKA, Sekretarieti ya IORA, Msalaba Mwekundu wa Uturuki, pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa mchango wao mkubwa na ushirikiano thabiti.
“Ni faraja kubwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mafunzo haya muhimu kwa maendeleo ya ukanda huu. Nawatakia kila la heri na natumai mmefurahia uwepo wenu hapa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla. Tunawakaribisha tena na tena,” amesema.




Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Mheshimiwa Bekir Gezer, alieleza kuwa Serikali ya Uturuki itaendelea kushirikiana na Tanzania, hasa katika masuala yahusuyo maafa. Amesisitiza kuwa nchi yao iko tayari kusaidia kwa kutoa vifaa muhimu vya kukabiliana na maafa.
Naye,Filiz Sahinci,Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la TİKA nchini Tanzania, amesema shirika hilo limejikita kusaidia juhudi za kukabiliana na maafa kwa kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika kutatua changamoto zinazotokana na maafa.
Mafunzo hayo yamehusisha wakufunzi kutoka Mataifa Kumi na Moja zilizopo kwenye Mwambao wa Bahari ya Hindi na yameweka msingi muhimu wa kuimarisha utayari wa jamii dhidi ya majanga na magonjwa ya kuambukiza, hususan katika mazingira ya baada ya maafa.
More Stories
WMA yafikia asilimia 96 utekelezaji mpango kazi wa Mwaka
Kamishna wa umeme na nishati jadidifu afanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya umeme jijini Dar
Majaliwa:Wanufaikaji Mikopo ya Elimu ya Juu kuongezeka