January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuijengea uwezo hospitali ya rufaa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Musoma

Fresha Kinasa, TimesMajira Online, Musoma

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amemhakikishia Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo kuwa, Serikali imejidhatiti kuongeza ufanisi na uwezo wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Musoma kuipatia chuo cha mafunzo ya afya.

Pia inalenga kuendelea kuthamini na kuenzi kwa dhati kazi iliyofanywa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Amesema tayari ameshafanya majadiliano na Waziri wa Elimu Prof. Adolf Mkenda na kulibariki ambapo wameishapata chuo ambacho kipo tayari kwenda kufungua tawi Mjini Musoma mkoani Mara.

Ummy ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma Juni 10, 2024 kufuatia Prof. Muhongo kumuomba Waziri kuanzishwe kozi ya Medicine katika Hospital ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Musoma ili kutatua changamoto ya Watumishi wa sekta ya Afya kwa kupata madkatari, Wauguzi na manesi.

“Kwa kuanzia, tuanze na taaluma za manesi,wauguzi na baadaye Medicine, nimuongezee Waziri duniani kote hospitali zote kubwa ni zile zinazotibu,kufundisha na kufanya utafiti (Teaching Hospital) na nimuombe kozi ianze mwakani,”amesema Prof. Muhongo.

” Lakini tunajiona kama serikali tunaowajibu wa kuendelea kuthamini na kuenzi kazi kubwa na nzuri ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere”amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema kuwa anakubaliana na ushauri wa Prof.Muhongo alioutoa kuwa huduma za afya ziendane sambamba na tiba, mafunzo pamoja na tafiti ambapo amesema serikali itaendelea kulisisitiza jambo hilo katika hospitali zote kubwa nchini.