June 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuendelea na utoaji mafunzo ya Mtaala ulioboreshwa kwa walimu wote

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe

SERIKALI itaendelea kutoa mafunzo ya Mtaala ulioboreshwa kwa walimu wote nchini ili kuhakikisha wanakuwa bora katika eneo la ufundishaji na ujifunzaji shuleni, huku walimu wote waliopata mafunzo ya somo la elimu ya biashara nchi nzima wakitakiwa kuwa na mtazamo mpya katika kufundisha somo hilo.

Hayo yamesemwa Juni 11, 2025 na Naibu Katibu Mkuu Elimu kutoka Ofisi ya Rais na Utawala Bora TAMISEMI, Atupele Mwambene  aliyemwakilisha, Katibu Mkuu TAMISEMI, Adolf Nduguru  kwenye ufungaji wa mafunzo ya walimu wa ajira mpya wa somo la Elimu ya Biashara katika Mtaala ulioboreshwa katika Chuo cha Ualimu Korogwe, mkoani Tanga.

Mwambene amewataka kuhakikisha wanakuwa na mtazamo chanya katika kufundisha somo hilo la elimu ya biashara kwa kuhakikisha wanakwenda shuleni kuwafundisha walimu vyema ili waweze baadae kutumia somo hilo katika kujiajiri wenyewe kwa namna watakavyoweza kuwandaa .

“Hakikisheni mnakuwa na mtazamo chanya mnaporejea katika vituo vyenu vya kazi. Haya mafunzo yakalete mabadiliko kwa wanafunzi nchini, kwani maboresho katika mtaala umeweka masuala ambayo yatamsaidia mwanfunzi katika kujifunza vyema suala la biashara” amesema Mwambene.

Pia, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha elimu nchini ikiwemo kutoa ajira kwa walimu nchini pamoja na kuidhinisha fedha za mafunzo kwa walimu wote nchini na kuendelea kuimarisha sekta ya elimu.

Katika hatua nyingine, ameitaka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuhakikisha inaendelea kuimarisha mafunzo endelevu kazini (MEWAKA) kwa walimu wote ili waweze kuendelea kujifunza katika jumuiya za ujifunzaji, kuongeza ujuzi na uelewa wa  masomo kazini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba amewaasa walimu hao kuwa chanzo cha mabadiliko katika ufundishaji wao kwa somo hilo la elimu ya biashara,  na kusema kuwa mbinu walizojengewa katika mafunzo hayo wazitumie vyema katika kuhakikisha wanakuwa bora.

“Hakikisheni mnazingatia yote mliyofundishwa kwenye mafunzo haya.  Yatumieni vyema mnaprojea katika vituo vyenu vya kazi , naomba sana mzingatie yote mliyofundishwa ili mkalete mabadiliko” amesema Dkt. Komba.

Aidha, Dkt. Komba ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipatia TET fedha kutekeleza majukumu yake yakiwemo utoaji wa mafunzo na uandaaji na usambazaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Naye Afisa Elimu wa Korogwe  Mary Mmari amesema kuwa mafunzo hayo yana tija kwa walimu wote walioweza kuyapata, hivyo amewaomba walimu hao wakawe sehemu ya mabadiliko.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Shirika lisilo la kiserikali la EDUCATE, Nelson Musikula amesema, kama wadau wataendelea kutoa ushirikiano katika kuinua elimu nchini hasa katika somo la elimu ya biashara ili kuwezesha wanafunzi wote nchini, wanapata uelewa na kuweza kujifunza namna ya kuanzisha biashara.

Jumla ya walimu 1,913 wamepata mafunzo, ambapo katika kituo cha  Chuo cha Ualimu Tabora jumla ya walimu walikuwa  513, kituo cha Chuo cha Morogoro  ni   791, huku  Chuo cha Ualimu  Korogwe wakiwa  609.