Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kutoa fedha za kugharamia mradi wa kufua umeme kwa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) ili ukamilike kwa wakati.
Waziri Mkuu amesema hayo leo wakati alipotembelea na kukagua mradi huo uliopo Mto Rufiji, katika Mikoa ya Pwani na Morogoro, huku akifarijika kuona kazi yenye viwango na ubora inayofanywa na Kampuni ya Arab Contractors pamoja na Elsewedy Electric zote kutoka nchini Misri chini ya usimamizi wa TANESCO, TANROADS na Wizara ya Nishati.
“Wakandarasi wamenihakikishia kukamilisha ujenzi wa mradi kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili kutuachia mradi ambao utakua na ubora na thamani kama tulivyo kubaliana” amesema Majaliwa.
Mradi huo unaotarajiwa kukamilika June 2022 utaiwezesha nchi kupata umeme mwingi wa uhakika na gharama nafuu, utasambazwa nchi nzima huku ziada ikiuzwa nje ya nchi ili kulipatia taifa fedha za kigeni.
Mbali na fedha za kigeni mradi huu ambao mpaka sasa umeajiri Watanzania zaidi ya 6,000, utakapo kamilika utazalisha megawati 2,115 ambazo zikijumlishwa na megawati 1,500 zinazozalishwa na vyanzo mbalimbali kwa sasa, Tanzania itakuwa na umeme wa kutosha pamoja na ziada.
“Mradi huu ni moja ya juhudi za Serikali katika kupunguza gharama za umeme kwa wananchi kwani uzalishaji wake ni wa gharama nafuu tofauti na vyanzo vingine. Uniti moja ya umeme unaozalishwa kwa kutumia maji inagharimu shilingi 36 hadi shilingi 50 huku umeme unaotumia vyanzo vya mafuta uniti moja inazalishwa kwa gharama ya shilingi 440 hadi shilingi 600.” Anasema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Aidha, amesema Serikali imedhamiria kupeleka umeme hadi katika Vitogoji, ikiwa ni pamoja na vilivyopo visiwani akitolea mfano visiwa vya Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, na Ziwa Nyasa pamoja na visiwa vilivyopo kwenye ukanda wa Bahari ya Hindi huku umeme huo kusaidia maendeleo ya viwanda nchini.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito