January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuendelea kusimamia masoko ya mazao

Na Patrick Mabula,TimesMajira Online. Kahama

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema serikali itaendelea kusimamia masoko ya mazao ya wakulima waweze kunufaika na kilimo chao.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi mwishoni mwa wiki katika mikutano ya kampeni kwenye majimbo ya Ushetu, Msalala na Kahama mjini wilayani hapa amesema serikali itaendelea kusimamia kilimo na masoko ya mazao ya wakulima waweze kunufaika na kuwataka wapinzani kuacha kupotosha.

Akiwa katika Jimbo la Ushetu maarufu kwa kilimo cha mazao ya tumbaku, pamba, mahindi na karanga amewataka wakulima kuongeza tija katika kilimo na serikali, itaendelea kusimamia masoko ili wakulima wanufaike na mazao yao.

Majaliwa amesema mwaka huu, mazao ya wakulima bei yake imeporomoka kutokana na janga la ugonjwa wa Corona na kuwataka wasikate tamaa na waongeze tija katika kilimo na serikali, itasimamia masoko kuhakikisha wanapata bei stahiki na wananufaika na mazao yao.

Amesema serikali si mnunuzi wa mazao ya wakulima, kazi ambayo inafanya ni kuhakikisha inawadhamini wanunuzi na wadau mbalimbali, kuhakikisha wanapatiwa fedha na mabenki kwa lengo la kununua mazao yao katika masoko ya ndani na nje ya nchi.