Na Mwandishi wetu TimesMajira Online
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima amesema kuwa Serikali imejipanga kuendelea kuboresha na kusimamia utoaji huduma bora jamii kupitia idara ya ustawi wa jamii kwa lengo la kupunguza changamoto eneo hili zikiwemo wimbi la watoto wa wanaoishi kwenye mazingira magumu na hatarishi pia na wale wanaokinzana na sheria. Maboresho haya ni muhimu kwa lengo la kuwa na taifa lenye watu wanaoishi kwa amani na utulivu.
Dkt.Gwajima amebainisha hayo katika mkutano mkuu wa chama cha wataalamu na watoa huduma za ustawi wa jamii ( TASWO ) na kongamano la kitaifa Tanzania Bara na Visiwani lililofanyika mapema leo 24 Novemba 2021 jijini Mwanza lililohudhuriwa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dr Nandera Mhando na Afisa Ustawi wa Jamii toka Ofisi ya Rais Tamisemi Bi. Nkinda Shekalaghe pia na Afisa Ustawi wa Jamii mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Philbert Kawemana.
Dk Gwajima amesema tayari Wizara imekamilisha kufanya mapitio ya Sera ya Wazee ya mwaka 2003 na kuandaa andiko la wasilisho serikalini kwenye baraza la mawaziri kwa hatua zaidi.
Amesema Serikali imeendelea kufanya utambuzi wa kaya masikini na kutoa bima za afya na matibabu bila malipo kwa wazee tangu mwaka 2015 ambapo hadi kufikia Juni, 2021 jumla Wazee wasiojiweza 2,203,414 (1,198,338 wakiwa ni wanawake na 1,005,076 wakiwa ni wanaume) walitambuliwa.
Amesema Jumla ya Wazee 1,256,544 wameweza kupatiwa kadi za bima ya Afya na matibabu bila malipo na Hadi kufikia sasa kuna jumla ya madirisha ya huduma kwa Wazee 2,335 katika hospitali na vituo vya afya kwa ajili ya kuharakisha na kutoa huduma za afya stahiki kwa Wazee nchi nzima.
Ameongeza pia kuwa serikali imeendelea na utoaji huduma ya makazi kwa wazee wasiojiweza kwa kushirikiana na wadau na hadi sasa kuna jumla ya makazi ya Wazee 15 ambayo yana jumla ya Wazee 291, kati yao Wanaume ni 180 na Wanawake ni 111.
Aidha, ameeleza wizara imeendelea kuratibu na kusimamia huduma katika makazi binafsi ya Wazee hapa nchini, ambapo hivi sasa kuna jumla ya makazi binafsi ya Wazee 14 yanayotoa huduma kwa Wazee 451, kati yao Wazee 216 ni wanaume na 235 ni wanawake.
Dkt. Gwajima ameweka wazi kuwa serikali inaendelea kutekeleza jukumu la ulinzi na usalama wa Watoto walio katika mazingira hatarishi ambapo kupitia Mfuko wa ABBOT wizara ya afya imefanikisha ujenzi wa Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo yaliyoko katika Jiji la Dodoma yenye uwezo wa kuhudumia watoto 250, hivi sasa kuna jumla ya Watoto 55, kati yao wakiume ni 34 na wakike ni 21
Amesema hadi sasa kuna jumla ya watoto wanaoishi na kufanyakazi mitaani 5,390 (1,538 wasichana na 3,852 wavulana) waliotambuliwa katika Mikoa ya Mwanza, Arusha, Iringa, Mbeya and Dodoma.
Amesema Kati ya watoto hao, jumla ya Watoto 135 (43 Ke and 92 Me) waliweza kuunganishwa na familia zao, watoto 821 (302 Ke and 519 Me) waliweza kupewa vifaa saidizi na kupelekwa shuleni, na watoto 75 (17 Ke and 58 Me) walipewa mafunzo ya uanagenzi.
Aidha Wizara imeweza kusajili jumla ya vituo 301 vya kulelea Watoto Wadogo mchana vilivyosajiliwa na Vituo 33 vya kulelea Watoto Wachanga viliweza kupata usajili. Idadi hiyo inapelekea kuwa na jumla ya Vituo vya kulelea watoto wadogo mchana 1,844 kwa nchi nzima. Katika vituo vya kulelea Watoto Wadogo mchana vilivyosajiliwa kuna jumla ya Watoto 163,394 (85,175 Me na 78,219 Ke).
Amesema ongezeko la watoto wa mitaani limechangiwa na mambo mbalimbali yanayojitokeza katika jamii kama vile kutengana kwa wazazi, wazazi kujikita zaidi katika utafutaji maisha na uzalishaji mali, umasikini wa kaya, vifo vya wazazi na walezi na msukumo wa makundi rika.
Dkt Gwajima ametoa wito kwa wadau wote ikiwemo halmashauri nchini kuangalia uwezekano wa kutumia mwongozo wa kitaifa wa watu wanaojitolea kusaidia kuajiri wataalam wa ustawi wa jamii katika ngazi mbalimbali ili kukidhi utoaji wa huduma kwa makundi maalumu yenye uhitaji ikiwemo wazee na watoto.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa