January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuboresha uzalishaji zao la parachichi nchini

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Rungwe

SERIKALI imeamua kukiboresha kilimo cha zao la parachichi nchini katika halmashauri zinazolima zao hilo kwa kuweka mipango na mikakati ya kuongeza tija ya uzalishaji ili kuwasaidia wakulima kuachana na mazoea na kuwaunganisha wawekezaji na masoko ya nje ya nchi hususan Afrika Kusini .

Imeelezwa kuwa licha ya changamoto hizo Wizara ya Kilimo imepanua wigo ikiwa ni pamoja na maandalizi ya shamba, upatikanaji wa mbegu na pembejeo zake, uhifadhi pamoja na masoko.

Hayo yamesemwa leo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kaasim Majaliwa  wakati alipotembelea mashamba ya maparachichi pamoja na kiwanda cha kuchakata zao hilo.

Aidha Majaliwa amesema kuwa wakulima wote ambao wapo tayari waanze kulima zao la parachichi, serikali imeweka utaratibu mzuri wa kilimo cha zao hilo.

Hata hivyo amesema kama hiyo haitoshi wameamua kuunda kurugenzi ya zao hilo ndani ya wizara ambapo itakuwa inashughulikia mambo ya bustani.

Akielezea zaidi Majaliwa amewataka wakulima kuendelea kulima zao hilo na kwamba serikali ipo pamoja nao, zao hilo limeingizwa kwenye utaratibu na Waziri wa Kilimo ataanza ziara ya kuwatembelea wakulima .

“Natoa maagizo kwa maafisa kilimo wote kuanzia wa mkoa na wale waliopo wilayani kuhakikisha wakulima wanapata msaada wa kitaalamu ili waendelee kulima zao hili, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kuwa changamoto kubwa kwenye uwekezaji wa zao la parachichi ilikuwa ni uhakika wa soko hivyo zao hilo kuharibikia nyumbani kutokana na kukosa soko.

Mbunge wa  Jimbo la Rungwe, Antony Mwantona amesema kuwa wananchi wa wilaya hiyo wana changamoto ya wakulima wa viazi anaomba wizara husika kusaidia suala la Rumbesa kwenye mazao ya viazi katika eneo la Ntokela .