May 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali Kuboresha Elimu ya Ufundi: Shule 55 Kubadilishwa Kuwa Sekondari za Amali

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online – Dodoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania itawezesha upanuzi wa shule 55 za sekondari kuwa sekondari za amali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali nchini.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma, Prof. Mkenda amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha utoaji wa elimu ya amali katika shule za sekondari, sambamba na kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023.

Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha elimu ya ualimu kwa kujenga miundombinu na kuweka vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia katika Chuo cha Ualimu Mtwara Kawaida (K) na Chuo cha Ualimu Mtwara Ufundi (U), ili kuviwezesha kuwa vyuo vinavyotoa mafunzo ya ualimu wa amali.

Pia Serikali itaongeza fursa za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kwa kusajili vyuo 100 vipya, ikiwemo vyuo vya elimu ya ufundi 30 na vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi 70. Hatua hii itaifanya nchi kuwa na jumla ya vyuo 504 vya elimu ya ufundi na vyuo 898 vya mafunzo ya ufundi stadi.

Aidha, Serikali inatarajia kusajili shule 100 za sekondari za ufundi na kudahili wanafunzi 265,000 wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, ambapo wanafunzi 190,000 watajiunga na vyuo vya elimu ya ufundi na 75,000 katika vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 43 ikilinganishwa na udahili wa mwaka wa 2024/2025.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa Serikali itatoa ithibati kwa vyuo 70 vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, na kufanya jumla ya vyuo vilivyopata ithibati kufikia 370, hatua itakayosaidia kudhibiti ubora wa mafunzo yanayotolewa.

Serikali pia itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya vyuo vya elimu ya ufundi, mafunzo ya ufundi stadi pamoja na vyuo vya maendeleo ya wananchi, ikiwa ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa awamu ya pili ya vyuo 64 vya VETA vya wilaya na chuo kimoja cha Mkoa wa Songwe.

Prof. Mkenda amesema ujenzi wa vyuo vitano vipya vya ufundi (Polytechnic Colleges) utaanza katika mikoa ya Rukwa, Kigoma, Mtwara, Morogoro na Zanzibar. Vilevile, Serikali itajenga hosteli tatu katika vyuo vya maendeleo ya wananchi kwa lengo la kuongeza udahili wa wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali.

Katika juhudi za kuboresha miundombinu, Serikali itakarabati vyuo 54 vya maendeleo ya wananchi na kuendelea na awamu ya pili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Dodoma, ambapo ujenzi huo utahusisha mabweni mawili yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 600 kwa wakati mmoja, maktaba yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,000, karakana mbili kwa wanafunzi 300, nyumba 10 za watumishi na ukuta kuzunguka chuo.

Aidha, Serikali itaendelea na ujenzi wa maktaba ya kisasa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,000 kwa wakati mmoja katika Chuo cha Ufundi Arusha, pamoja na kukamilisha ujenzi wa mtambo wa kufua umeme kwa kutumia nguvu za maji katika Kituo cha Mafunzo cha Kikuletwa. Mtambo huo utasaidia kutoa mafunzo kwa vitendo na kuwezesha upanuzi wa maabara ya udongo ili kuhudumia wanafunzi wengi zaidi.

Pia, Serikali itaendelea na ujenzi wa mabweni mawili yatakayoweza kuhudumia jumla ya wanafunzi 1,536, wakiwemo wanaume 768 na wanawake 768.