Na Jackline Martin, TimesMajira Online
SERIKALI kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema itaanzisha skimu za umwagiliaji katika mashamba ya malisho ya Vikuge na Langwira, pamoja na ranchi za NARCO za Kongwa na Mzeri; Kujenga mabwawa na visima virefu kwa ajili ya maji ya mifugo; kuanzisha mashamba darasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Wizara; na Kujenga maghala ya kuhifadhi malisho na vyakula vya mifugo
Pia inatarajia Kukusanya maoni ya wadau na kufanya tathmini ya uanzishaji wa Mamlaka ya Kusimamia na Kuendeleza Miundombinu ya Mifugo na Uvuvi nchini na vilevile kuendesha kampeni ya kudhibiti magonjwa kwa kujenga majosho, kununua dawa za kuogesha mifugo na kusambaza dozi za chanjo katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo ameyasema Waziri wa mifugo na uvuvi Abdallah Ulega wakati akiwasilisha ripoti kuhusu makadirio Ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara ya mifugo na uvuvi kwa mwaka 2023/2024 bungeni leo Jijini Dar es Salaam.
“Ni matumaini ya serikali hii kwamba endapo suala la malisho litaboreka, migogoro inayojitokeza mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji itapungua na badala ya kugombana, watafanya biashara pamoja. Kwa malisho hayo mazuri, mifugo yetu itakuwa na afya nzuri zaidi, itauzwa kwa bei nzuri na biashara ya mifugo itakuwa bora zaidi kwa wafugaji.” Amesema Ulega
Aidha Waziri Ulega amesema kuwa Serikali itawawezesha wavuvi na wafugaji wa Samaki kupata pembejeo na zana za kisasa za uvuvi ikiwemo boti na vizimba kupitia programu ya mkopo nafuu (ECF); kwa kujenga mialo, masoko na kujenga vituo vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi.
Aidha Mhe. Ulega amssema kuwa Serikali inatarajia kujenga Minada mipya na kukarabati iliyopo na kufunga Mizani kwenye Minada ili kupata thamani halisi ya Mifugo na kuweka wazi kuwa ujenzi wa Bandari ya uvuvi Ya Kilwa Masoko pamoja na Ununuzi wa Meli tatu (3) za uvuvi wa Bahari Kuu unaendelea ili kuongeza mazao ya samaki.
Vilevile amesema lengo ni Kuimarisha Vituo vya Ufugaji wa Samaki kwa kukarabati na kuongeza Miundombinu ili kuzalisha Vifaranga zaidi vya Samaki, Kupandikiza Vifaranga vya Samaki katika Mabwawa ya asili na kutoa mafunzo kwa wakulima wa Mwani sambamba na Maabara ya Taifa ya Uvuvi kwa kuiwezesha kuwa na vifaa vya kufanya Uchunguzi wa Sampuli na Kufanya kaguzi za kuhakiki ubora wa Mazao ya Uvuvi
“katika mwaka 2022/2023, idadi ya miundombinu ya ukuzaji viumbe maji imefikia mabwawa 32,878, vizimba 993, vitotoleshi 39 vya kuzalisha vifaranga na viwanda nane (8) vya kutengeneza chakula cha samaki. Aidha, uzalishaji wa mazao mbalimbali ya ukuzaji viumbe maji ulifikia tani 33,525.5 na vifaranga vya samaki 35,967,180 ambapo kati ya hivyo, vifaranga 31,000 vimepandikizwa katika malambo mbalimbali nchini ili kuongeza upatikanaji wa samaki.”
Kadhalika amesema Serikali inakusudia kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi mahususi kwa ajili ya kusimamia na kuendeleza Rasilimali za Uvuvi kwa lengo la kuongeza ufanisi katika Usimamizi, ulinzi na uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi ambapo itawezesha kupunguza au kuondoa changamoto zinazoikabili Sekta ya Uvuvi ikiwa ni pamoja na kukabiliana na Uvuvi haramu.
“Tunakusudia kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi ambayo kazi yake mahususi itakuwa ni kwa ajili ya kusimamia na kuendeleza rasilimali za uvuvi kwa lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi, ulinzi na uendelezaji wa rasilimali za uvuvi. Ushauri wa kuanzishwa kwa chombo hiki ulianzia humuhumu bungeni na serikali imeona kuna mantiki na faida kubwa kwenye kuanzisha chombo hiki.” Amesema
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu