January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali itaendelea kushirikiana na Sekta binafsi ili kuongeza soko la ajira – Majaliwa

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online DSM

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa ametoa wito kwa waajiri nchini kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha malengo ya kukuza ujuzi na kuongeza soko la ajira yanafanikiwa kwa mustakabali wa Taifa.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwatambua na kuwapongeza waajiri na wadau wanaoshirikiana na Serikali katika kukuza na kuendeleza ujuzi kwa wanafunzi walioko vyuoni na waliohitimu.

Amesema maendeleo ya uchumi wa nchi yoyote yanategemea nguvu kazi yenye ujuzi hivyo mchango wa wadau kama waajiri ni muhimu katika kufanikisha hilo.

“Niwapongeze waajiri kwa ushiriki wenu katika kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo, hii ni pamoja na uanagenzi. Aidha nawapongeza kwa ushiriki wenu katika katika kuaandaa mitaala inayotumika katika Vyuo na Taasisi za Elimu ya Ufundi na mafunzo ya Ufundi Stadi”, amesema Majaliwa.

Ameongeza Serikali inatambua na inathamini juhudi zinazofanywa na waajiri hao katika kuliwezesha Taifa kukabiliana na changamoto ya ajira na kuiwezesha nchi kuwa na rasilimaliwatu yenye ujuzi.

“Niwahakikishie waajiri Serikali inathamini mchango wenu katika kuliwezesha taifa kukabiliana na changamoto ya ajira. Kazi mnayoifanya imedhihirisha uzalendo wa hali ya juu na inaonesha wazi kuwa waajiri mnaunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi yenye rasilimaliwatu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kujenga uchumi imara katika nchi,”ameongeza Waziri Mkuu Majaliwa.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amemweleza Waziri Mkuu kuwa Wizara itaendelea kusimamia Mkakati wa Taifa wa uendelezaji wa ujuzi 2016/17 -2025/26 ambao moja ya malengo yake ni kuwa na ushirikiano kati ya waajiri wadau na vyuo au taasisi za elimu.

“Tumekamilisha tracer study ya kutambua hali ya ajira kwa wahitimu wa vyuo vyetu vya ufundi iwapo wameajiriwa uwezo wao wa kazi na mapungufu.Hii itasaidia kuboresha mitaala yetu na hatimaye kuboresha elimu itolewayo,”amesema Prof. Mkenda.

Nae Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Dkt. Adolf Rutayuga amesema mafunzo yanayotolewa kwenye vyuo na Taasisi za elimu na mafunzo ya ufundi stadi yanaongozwa na mahitaji ya soko la ajira hivyo kukutana na waajiri ni fursa nzuri katika kukumbushana nafasi yao katika kukuza ujuzi nchini.

Kauli mbiu ya hafla ya kuwatambua na kuwapongeza waajiri na wadau wanaoshirikiana na Serikali katika kukuza na kuendeleza ujuzi kwa wanafunzi walioko vyuoni na waliohitimu kwa mwaka 2023 ilikuwa Kuimarisha Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa uzalishaji wa wafanyakazi wenye ujuzi nchini Tanzania.