March 30, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali ipo kwenye maandalizi ya TASAF III,ambao hawajainuka kiuchumi TASAF II kupewa kipaumbele

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

SERIKALI imesema wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini awamu ya pili (TASAF II) ambao hawajafanikiwa kiuçhumi katika awamu ya pili ya Mpango ,watapewa kipaumbele katika Mpango wa Tatu unaotarajiwa kuanza 2026-2030.

Aidha amesema walengwa waliotambuliwa ni zaidi ya milioni 1.3 ambapo waliohitimu katika Mpango huo wapo laki nne na kati yao wamefanyiwa tathimini na kwamba kati ya hao walengwa laki moja walionekana wana hali duni.

Naibu Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deus Sangu ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Fakharia Shomari Khamis ambaye katika swali lake la nyongeza alitaka kujua kama walengwa wa TASAF II ambao wameshatolewa kwenye mpango huo wa pili na bado hawajafanikiwa kiuchumi kama wataingizwa katika Mpango ujao ili watengeneze maisha yao.

Akijibu swali hilo,Naibu Waziri Sangu amesema kuwa hao waliobainika kwamba bado wana hali duni,Serikali haikuwaacha isipokuwa imewapa mkono wa kwakheri ya shilingi 350,000 na na Elimu ya ujasiriamali huku akisema ni Imani ya Serikali kwamba hao walio-‘graduate’ pia wana fursa nyingine awamu ijayo ya 2026-2030 ambapo watapewa kipaumbele kulingana na hali zao mara baada ya kufanyiwa tathimini.

Aidha Sangu amesema
, Serikali ipo kwenye maandalizi ya kuendelea na Kipindi cha Tatu cha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (PSSN) ambacho utekelezaji wake utakuwa wa miaka 5 kuanzia mwaka 2026 hadi mwaka 2030 katika maeneo yote ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo ,lengo la Kipindi cha Tatu cha Mpango ni kuendelea kupambana na umaskini wa Kaya za Walengwa zenye hali duni ikiwa ni pamoja na makundi maalum ya watoto na wazee na kwamba ,Mpango unalenga kuzijengea kaya hizi ujuzi wa ujasiriamali ili waweze kuwa na misingi ya kujitegemea.

” Mpango huu utaendelea kutumia dhana ya ushirikishwaji jamii ili kufikia malengo ya kupambana na umaskini.” amesisitiza Sangu