January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali imetakiwa kufufua viwanda mkoani Mwanza

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Serikali imetakiwa kufufua viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali yanayotokana na mifugo,uvuvi na kilimo mkoani Mwanza ili kuchochea uchumi wa taifa na kufanya Mkoa huo kuwa lango kuu la biashara.

Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara,Kilimo na Mifugo Deodatus Mwanyika katika kikao cha kujitambulisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makala katika ziara yao ya siku mbili mkoani hapa ya kutembelea Chuo cha Elimu ya Biashara(CBE).

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara,Kilimo na Mifugo Deodatus Mwanyika

Mwanyika ameeleza kuwa awali ili fahamika kuwa Mkoa wa Mwanza kuwa na viwanda ambapo ukisema nguo ni Mwatex,mafuta mazuri yote yalikuwa yanatoka katika Mkoa huo lakini sasa viwanda vyote vimekufa.

Ameeleza kuwa Mkoa wa Mwanza ulikuwa na viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi samaki lakini karibu vyote vimefungwa vimebaki vitatu pekee yake.

“Serikali ifufue viwanda hivyo na sisi Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara, Uvuvi na Kilimo tutasimamia kikubwa ni kufufua hasa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo,ufugaji na uvuvi,”ameeleza Mwanyika.

Hata hivyo ameeleza kuwa Rais Samia ametumia fedha kununua ndege kubwa ya mizigo ambayo inaweza kuwa chachu ya kufufua viwanda kwa kupeleka mazao moja kwa moja kwenye masoko.

“Kamati ya Bunge tupange tutembelee tena Mwanza tuje tuone hizi changamoto zinatatuliwaje,”.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makala ameeleza kuwa kipaumbele cha Mkoa wa Mwanza ni kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ya kuwezesha kufanya biashara kwani ni Mkoa wa pili katika kuchangia pato la taifa.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makala

“Rais amenunua ndege ya mizigo na imeisha kua hapa mara mbili lakini inakosa mzigo wa kutosha kwaio moja ya agenda yetu ni kurejesha Ziwa Victoria lenye samaki kwaio tunayo kazi kubwa na kipaumbele chetu ni kutoa elimu lakini kuwa na ufugaji wa samaki na wakati huo tukisubili zile operesheni na mikakati tulioiweka inatekelezwa,”ameeleza Makala.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza ELIKANA Baladya ameeleza kuwa sekta ya kilimo mkoani Mwanza ndio inayochangia asilimia kubwa ya shughuli mkoani hapa huku uvuvi ikiwa ni muhimu kwa maisha ya wanamwanza.

Ameeleza kuwa serikali imechukua hatua ya kutekeleza mpango wa BBT kwenye sekta ya uvuvi ambapo vijana wa makundi mbalimbali yamewezeshwa kufuga kwa njia ya vizimba.

“Serikali sasa hivi inaendelea na utekelezaji wa vizimba takribani 600, ambavyo vitatolewa kwa vijana wa vikundi mbalimbali ambavyo vinalenga kupunguza tatizo la ajira,”ameeleza.

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Elikana Baladya

Pia ameeleza kuwa sekta ya uvuvi Ina fursa nyingi ambazo wanaMwanza na taifa kwa ujumla wanahitaji kuzitumia.

”Kwa mfano fursa ya utengenezaji vizimba lakini kuna fursa ya kuanzisha viwanda ambavyo vinazalisha chakula kwa ajili ya samaki pia fursa ya ya kuanzisha vyumba vya kuhifadhia baridi(cold room) kwa ajili ya kutunza samaki zipo fursa nyingi ambazo kama tutazitumia vizuri itatusaidia sana kuondokana na hali ya umaskini na kuboresha maisha ya jamii,”amesema.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amesema Wizara itaendelea kushirikiana na Mkoa wa Mwanza katika fursa mbalimbali ikiwemo za biashara,uvuvi, mifugo na kilimo.

Baadhi ya washiriki wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara,Mifugo na Kilimo