March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali imepiga hatua matumizi ya teknolojia katika afya

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online-Dar

SERIKALI imesema imepiga hatua katika matumizi ya teknolojia ya kisasa na data pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.

Kauli hiyo imetolewa Oktoba 1,2025 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, wakati akifungua mkutano wa 12 wa Afya Tanzania (THS) unafanyika kwa siku tatu,ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar-es-Salaam.

Dkt. Shekalaghe amesema serikali imeweka mkazo katika uwekezaji wa mifumo ya kisasa ya afya, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kauli mbiu ya mwaka huu inayolenga matumizi ya data na teknolojia kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma kwa wote.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, tunao mfumo jumuishi wa rekodi za matibabu za kielektroniki,unao unganisha taarifa za mgonjwa kuanzia ngazi ya jamii, vituo vya afya, hospitali za wilaya hadi taifa,” amesema Dkt. Shekalaghe.

Aidha, amesema kuwa mfumo huo unarahisisha ufuatiliaji wa huduma na kuwezesha madaktari kupata taarifa sahihi za wagonjwa kwa haraka, jambo linalosaidia kuokoa maisha na kuboresha ubora wa huduma.

Akizungumzia teknolojia nyingine bunifu, Dkt. Shekalaghe alitaja mfumo wa M-Mama kuwa mfano bora wa mafanikio ya matumizi ya teknolojia katika sekta ya afya.

Amesema mfumo huo wa kidijitali unaratibu huduma ya usafiri wa dharura kwa mama wajawazito na watoto wachanga walioko hatarini, kupitia namba maalum ya bure 155.

“M-Mama sasa ni mfumo rasmi wa kitaifa wa usafiri wa dharura kwa kina mama na unahudumia mikoa yote ya Tanzania. Unatarajiwa kuwasaidia wanawake na watoto wachanga takribani 50,000 kila mwaka kupata huduma wanazozihitaji,” amesema.

Aidha aliwahimiza washirika na wadau wa sekta ya afya kuendelea kushirikiana na serikali katika kuimarisha mifumo ya afya, akisema kuwa mkutano wa THS si jukwaa la kawaida bali ni sehemu muhimu ya ushirikiano, uwajibikaji na ubunifu katika sekta hiyo nyeti.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar,Dkt Salim Slim,akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, amesema Zanzibar pia imepiga hatua kisekta kutokana na mchango wa wadau katika matumizi sahihi ya data na teknolojia kuboresha huduma kwa wananchi.

Naye Mkurungezi wa Tehama kutoka Wizara ya afya ,Silvanus Ilomo,amesema Tanzania imekuwa ni nchi moja wapo ambayo inafanya vizuri sana katika eneo la teknolojia katika afya .

“Tumekuwa na uwekezaji mkubwa wa matumizi ya tehama katika sekta ya afya kuanzia ngazi ya kaya hadi ya taifa,kwani ipo mifumo ambayo imewekezwa inayoweza kukusanya takwimu kuanzia ngazi ya kaya hadi ngazi ya Taifa.

Amesema mifumo hiyo imekuwa ikikusanya taarifa mbalimbali ambazo zinakwenda kuisaidia Serikali kufanya maamuzi ya mambo mbalimbali ili kuboresha zaidi sekta ya afya.