January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali haita wavumilia watumushi wanaokiuka maadili

Na Sophia Fundi, Timesmajira Online,Karatu

Mkuu wa Wilaya ya Karatu mkoani Arusha Dadi Kolimba amesema kuwa serikali haitawavumilia watumishi wote wanaokiuka maadili ya kazi na kufanya kazi wanavyotaka wao.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu Mkuu huyo wa Wilaya Kolimba amewataka kila mtumishi kufanya kazi katika idara yake kwa kufuata taratibu,kanuni na maadili ya kazi ikiwemo muda wa kuigia kazini na kutoka.

Makamu Mwenyekiti Halmashauri ya Karatu John Bayo akizungumza na madiwani katika kikao Cha Baraza la Madiwani

Pia amewataka watumishi kuwa na nidhamu kazini ambapo amesema ni jukumu lao kuwahudumia wananchi kwa kusikiliza malalamiko yao kwani wameingia mkataba na serikali ya kuwaudumia wananchi wake.

“Ikumbukwe kuwa tumepewa jukumu la kuwatumikia wananchi katika majukumu yetu ya kiutumishi ambaye hatoweza kufanya hivyo serikali haitamvumilia,”amesema Kolimba.

Amemtaka Ofisa Utumishi kuwapeleka mahakamani watendaji wote waliokula fedha za umma na kuwafungulia mashtaka yanayoeleweka ya kuwatia hatiani.

Amesema kesi nyingi zinazofunguliwa na Halmashauri washitakiwa wamekuwa wakishinda hiyo ni kutokana na kuwafungulia mashtaka malaini jambo ambalo linawafanya kushinda.

“Tafuteni vifungu vya kuwatia hatiani haiwezekani mtumishi anakula fedha za umma,unampeleka mahakamani halafu anashinda ni uzembe wetu,”amesema Kolimba.

Amewahimiza Madiwani kuendelea kushirikiana na wataalam katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri huku akiwapongeza kwani ameona mabadiliko katika makusanyo ya mapato hayo kwa kuvuka asilimia katika ukusanyaji wa robo ya mwaka kwa kufikia asilimia zaidi ya 47.

“Mnaenda vizuri katika makusanyo ya mapato ya Halmashauri mpaka sasa tuko asilimia zaidi ya 47 katika robo ya mwaka msibweteke endeleeni na kasi mliyonayo tuweze kukamilisha miradi ya maendeleo,”amesema Kolimba.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo John Bayo kwa niaba ya Mwenyekiti amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa jitihada zake za kuwasimamia watumishi na kuwapa maelekezo ya kiutendaji.

“Mkuu wa Wilaya tunakupongeza kwa usimamizi wako wa kuwasimamia watendaji wa serikali ndani ya Wilaya na kuwapa maelekezo ya kiutendaji ni kwa usimamizi wako hadi leo tunajivunia kukusanya mapato ya Halmashauri kwa kuvuka asilimia katika robo ya mwaka,tunaahidi kukupa ushirikiano wewe pamoja na wataalam katika kuendeleza gurudumu la maendeleo ya Wilaya yetu,” amesema Bayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wilaya ya Karatu Juma Hokororo amewaomba Madiwani kushirikiana na wataalam katika Kata zao kwa kusimamia miradi yote inayotekelezwa na serikali.

Amewaomba madiwani kuhakikisha katika majukwaa yao wanatoa idadi ya miradi inayotekelezwa na serikali kwani imetoa fedha nyingi katika kutekeleza miradi ya maendeleo ndani ya Wilaya.