Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewataka watu wote wenye tabia za kutoa taarifa kwa umma kuhusiana na mambo yanayoendelea nchini kutambua kuwa wanakwenda kinyume cha taratibu wa mfumo wa Serikali na itifaki yake.
Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema hayo leo wakati akielezea kuhusu makundi ya watu ambao yameibuka katika jamii huku yakijipa mamlaka ya kutoa taarifa kwa umma wakati hawana mamlaka hayo.
“Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na tabia mpya ya baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii au maeneo mengine ya nchi kujitolea tu taarifa, nyingine zinahusu Serikali, nyingine taasisi za umma, bila kuzingatia misingi ya utoaji wa taarifa.
“Kama juzi ambavyo Mheshimiwa Rais alivyosema, alitoa maelekezo na maagizo kwa kwa Serikali, viongozi katika taasisi za utumishi wa umma watoe taarifa kwa umma, waeleze miradi waeleze matukio yanavyotokea katika taasisi zao. Hivyo niendelee kusisitiza tena kwamba, Serikali ina utaratibu wake wa kutoa taarifa mbalimbali, hivyo kwa watu ambao hawahusiki na taratibu hizo hawapaswi kuingilia huo mfumo na hiyo itifaki.
“Kama ilivyo kwenye maeneo mbalimbali hata kwenye maeneo ya magonjwa ya kuambukiza, magonjwa mbalimbali ya milipuko zipo taratibu kwenye sheria ya huduma au sheria ya afya ya jamii zimeeleza kwa mfano ni kiongozi wa aina gani ambaye anapaswa kutoa taarifa katika sekta ya afya.
“Vilevile tunakumbuka mfano mwaka jana, Tanzania ilipopata wagonjwa wa Corona wakatangazwa wakati ule Mheshimiwa Rais alitoa itifaki ya viongozi ambao watasemea maradhi haya ambapo viongozi hao ni pamoja na yeye mwenyewe, Waziri Mkuu, Waziri wa Afya na Msemaji Mkuu wa Serikali.
“Sasa tunashukuru kwamba, ugonjwa wa Corona tumeendelea kuudhibiti, lakini vile vile kama tulivyosema mara kadhaa kutokana na mwingiliano na wenzetu huko duniani, tunapaswa kuendelea kuchukua tahadhari za dhati kabisa, na Watanzania wengi wameendelea kuchukua tahadhari, lakini Mheshimiwa Rais ametuongoza vema kabisa kuwa watu wasiwe na hofu, watu wafanye mazoezi , wale vizuri, waendelee na majukumu yao ofisini, mashambani.
“Sasa umeibuka utaratibu mpya wa watu kujitokeza na kuanza kutoa takwimu zao kuhusu maradhi mbalimbali au kuhusu vifo au wagonjwa, ili kwa niaba ya Serikali naomba nisisitize siyo sahihi. Na tuviombe vyombo vya habari viachane kabisa na watu hao, kila mwanajamii, asasi za kijamii, viongozi wa kidini na taasisi nyingine wanapaswa kushiriki kutoa elimu kuhusu yale masuala ambayo yapo katika miongozo namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali na si kutoa takwimu ambazo hazina ukweli.
“Ni muhimu sana tusisite hilo, lakini utoaji wa takwimu na masuala mengine ya kisera yanapaswa kubaki kwa wataalam wetu ambao wana dhamana ya kufanya hivyo, niombe sana kwa jamii yetu kuzingatia hilo. Kwani mpaka sasa nchi yetu inaenda vizuri, tumeondoa hofu, tunafanya kazi, tupo kwenye mipira, matamasha, watanzania wapo kazini, maofisini, vyuoni na shuleni wanaendelea na majukumu yao, tunamshukuru Mungu sana kwa kuendelea kuwa pamoja nasi,”amesema.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa