Na Mary Margwe, Timesmajira Online-Simanjiro
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amemuagiza mkandarasi aliyejenga soko la madini ya vito Tanzanite Trading Centre mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro kukamilisha mradi huo ifikapo Septemba 15, Mwaka huu ili liweze kutoa huduma iliyokusudiwa.
Sendiga ameyasema wakati akiweka jiwe la msingi la jengo la soko la madini ya vito linalojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), hivyo ameliagiza kukamilisha jengo hilo ifikapo Septemba 15 mwaka 2025 kama mkataba wao unavyoonyesha ili liweze kufanya kazi iliyokusudiwa kwa wafanyabiashara wa madini na si vinginevyo.

Ameeleza kwamba soko hilo ambalo litakuwa na ghoroga Tano,likikamilika litaongeza thamani ya eneo hilo hivyo wana Simanjiro,Manyara na watanzania kwa ujumla wachangamkie fursa hiyo.
“Viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro natoa maelekezo kwenu hakikisheni viwanja vilivyopo jirani vinatolewa bila urasimu na watu wachangamke kujenga,” amesema Sendiga.
Msimamizi wa ujenzi wa soko hilo kutoka NHC, Anna Akyoo amesema kiasi cha bilioni 5.4 zimetumika kwa ajili ya ujenzi huo,na utekelezaji wake umefikia asilimia 98 na watahakikisha wanatekeleza maelezo ya Mkuu huyo wa Mkoa katika kukamilisha ujenzi huo.
Amesema mkataba wao umewaelekeza wamalize ghorofa mbili na ghorofa tatu za jengo hilo zilizobakia zikamilishwe na Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.
Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro,Gracian Makota, amesema,”Miradi ya maendeleo ni mingi hapa nchini ila wana Simanjiro tunashkuuru na pia mkuu wa mkoa amekuwa mwepesi kutusemea vyema wana Simanjiro juu ya jengo hili,”.

Mwenyekiti wa chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara, (Marema) Elisha Mnyawi amesema hivi sasa wamepata eneo sahihi la kuuza madini yao na watalipa kodi kwa uhakika.
Makamu Mwenyekiti wa chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (Tawoma) Rachel Njau,amesema ilikuwa hamu yao madini ya Tanzanite yanayopatikana pekee nchini kupata soko la uhakika.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi