January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sembi ang’ara TPC Open

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

NYOTA wa mchezo wa Gofu kutoka klabu ya TPC, George Sembi amefanikiwa kubakiza ubingwa wa michuano ya Gofu iliyoandaliwa na klabu hiyo nyumbani baada ya kuibuka kinara katika Mashindano ya Wazi ya TPC yaliyomalizika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya TPC Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Mchezaji huyo alitwaa ubingwa huo baada ya kupiga Mikwaju 147 akifuatiwa na Vicent Gulo wa TPC aliyefungana na Isihaka Daudi wa Lugalo ambaye ameshika nafasi ya Tatu kwa Mikwaju 149.

Kwa Upande wa Divisheni A, mshindi ni Nahuum Gabriel aliyepata Mikwaju ya jumla 147 akifuatiwa na Juma Mcharo aliyepiga Mikwaju ya jumla 148.

Mshindi wa Divisheni B ni Private Laurent Sangawe aliyepiga Mikwaju ya jumla 149 akifuatiwa na Private Haridi Shemdolwa wote wa Lugalo baada ya kupata Mikwaju ya jumla 152.

Sahif Kanabhai wa Arusha amefanikiwa kuibuka mshindi wa Divisheni C baada kupiga Mikwaju ya jumla 154 akifuatiwa na Issa Issa wa TPC aliyepiga Mikwaju ya jumla 147.

Kwa Upande wa Wanawake, mshindi ni Madina Iddi aliyepiga Mikwaju ya jumla  146 akifuatiwa na Neema Ulomi wote kutoka klabu ya Arusha huku Ashik Nanabhai wa Arusha akiibuka mshindi kwa upande wa Wazee.

Mshindi wa kwanza kwa watoto katika mashindano ya wazi ya Gofu ya TPC Ibrahim Gabriel (kulia) akikabidhiwa zawadi ya Baiskeli na Meneja wa klabu ya TPC, Merylize Buchanan katika sherehe zauUfungaji mashindano hayo.

Mshindi kwa upande wa Watoto ambao walicheza katika Viwanja tisa ni Zacharia George na katika Viwanja 18, mshindi ni Ibrahim Gabriel aliyepiga Mikwaju ya jumla 145.

Akizungumza katika Sherehe za Ufungaji wa Mashindano hayo, Nahodha wa klabu ya TPC ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa mashin dano hayo Jaffary Ally amezishukuru klabu zilizopeleka wachezaji katika mashindano hayo na kuwapongeza wachezaji wa kulipwa kwa utaalam walionyesha katika mashindano hayo.

Lakini kwa upande wa Meneja kitengo cha huduma za kifedha kwa sekta ya Kilimo Biashara kutoka Benki ya CRDB waliodhamini mashindano hayo, Ngenzi Sylivester amesema wao kama benchi watahakikisha wanaendelea kudhamini shughuli mbalimbali za michezo bila kubagua.