January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SELF Microfinance Fund kutoa mikopo kwa wakulima,wafugaji na wavuvi kukuza uchumi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MFUKO wa SELF Microfinance Fund, unatoa  fursa ya mikopo kwa ajili kwa wananchi hususan wakulima, Wafugaji na wavuvi  lengo likiwa ni kukuza Kilimo chao kutoka walipo na kufikia katika hatua yenye tija kiuchumi.

Akizungumza Agosti 6,2024 katika maonesho ya wakulima na Wafugaji (Nane nane), yanayofanyika Kitaifa viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Meneja Masoko na Uhamasishaji kutoka mfuko wa SELF Microfinance Fund, Linda Mshana amesema kuwa mfuko huo unawakopesha watu walipo kwenye vikundi, Taasisi, kampuni na mtu mmoja mmoja.

Meneja huyo amesema kuwa mfuko huo una mikopo mahususi kwa ajili yao ili kukuza Kilimo chao kutoka walipo na kufikia katika hatua kubwa na yenye ubora kupitia mikopo hiyo.

Mshana ameeleza kuwa kwa  mtu mmoja mmoja mfuko huo unatoa hadi milioni moja na kwamba unategemea mteja wao anahitaji kiasi gani.

Amesema kuwa mfuko huo pia unatoa mkopo kwa mazao ya muda mrefu na mfupi kuanzia mwaka mmoja hadi miwili.

“Tupo kwenye maonesho haya ambayo yanafanyika Dodoma tupo hapa kwa ajili ya kutoa fursa mbalimbali kwa wananchi hususan wakulima, Wafugaji na wavuvi,” amesema Mshana.

Aidha amewakaribisha wananchi waweze kutembelea banda hilo ambalo lipo ndani ya wizara ya fedha ili kupata fursa za mikopo mbalimbali.

Akizungumza mikopo ya kilimo amesema kuwa wanakaribisha vikundi ambavyo vinajihusisha na masuala ya kilimo kwa ajili ya kuapatiwa elimu ya mikopo ambayo wataipata bure lengo likiwa ni kuhakikisha wanapopata mikopo inaweza kuwaendeleza kiuchumi.

Mfuko wa SELF Microfinance Fund ni Taasisi ambayo ipo chini ya wizara ya fedha inatoa huduma za aina mbalimbali zikiwa mikopo, elimu ya fedha na huduma ya bima.