Na Lubango Mleka, Timesmajira Online.
KILA ifikapo Machi 16 hadi 22 ya kila mwaka Wananchi wote Dunia huazimisha wiki ya Maji, kama ilivyo kwa Mataifa mengine Tanzania pia huadhimisha siku hii ambapo kwa wilaya ya Igunga mkoani Tabora imeadhimisha siku hii kwa uzinduzi mkubwa wa upanuzi wa Mradi wa Majisafi na salama katika vijiji vya Mwabakima, Jogohya na Mwamashimba ambao unatoka katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza.
Katika kuadhimisha siku hiyo,Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Igunga (IGUWASA) imefanya shughuli mbalimbali, ikiwemo upandaji wa miti, kutoa Elimu mbalimbali ya Usafi wa Mazingira, Utunzaji wa vyanzo vya Maji, Huduma zinazotolewa na Mamlaka pamoja na uzinduzi mkubwa wa Mradi wa Maji katika kijiji cha Mwabakima.
Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Igunga mjini (IGUWASA), Eng Mwiyobela Hamphrey akisoma taarifa ya hali ya huduma ya maji katika vijiji vya Mwabakima, Jogohya na Mwamashimba katika uzinduzi wa mradi wa maji katika vijiji hivyo unaotoka katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza, alisema kuwa jina la Mradi huo ni upanuzi wa mtandao wa majisafi na salama katika vijiji vya Mwabakima, Jogohya na Mwamashimba.
Eng Hamphrey ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Hassan Suluhu na Wizara ya Maji kwa kuendelea kutoa fedha ili kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa Wananchi na kutatua kilio cha muda mrefu cha kukosekana kwa majisafi na salama katika maeneo ya Wananchi.
“Hali ya huduma ya maji katika vijiji vya Mwabakima, Jogohya na Mwamashimba ni miongoni mwa vijiji katika wilaya ya Igunga ambavyo vilikuwa vinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa kipindi cha muda mrefu,” amesema mhandisi Hamphrey.
Amesema, Wizara ya maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Igunga mjini (IGUWASA) imetekeleza mradi wa upanuzi wa mtandao wa majisafi na salama ili kuwawezesha Wananchi wa vijiji vya Mwabakima, Jogohya na Mwamashimba waweze kupata majisafi na salama yaliyokidhi viwango kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo.
Aidha, amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza Disemba 6, 2021 na kukamilika Disemba 6, 2022, huku makadirio ya gharama za utekelezaji wa mradi ikiwa ni takribani 830,706,695.00 na umetekelezwa kwa njia ya akaunti maalumu (FORCE ACCOUNT), chini ya usimamiz wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Igunga.
“Takribani Wanakijiji Elfu Kumi Mia Nne Thelathini na Moja (10,431) watafaidika na huduma ya majisifi na salama katika vijiji vya Mwabakima, Jogohya na Mwamashimba,” amesema Mhandisi Hamphrey.
Hata hivyo, amesema kazi zilizotekelezwa katika mradi huo ni ununuzi wa bomba HDPE kama ikiwemo kununua bomba HDPE 110mm PN 10 lenye urefu wa 17 km, HDPE 63mm PN 10 lenye urefu wa 7.5 km, HDPE 50mm PN 12 lenye urefu wa 4.5km, HDPE 32mm PN 12 lenye urefu wa 7.5kme na HDPE 25 mm PN 12 lenye urefu wa 15km.
“Pia tumenunua viungo vya Bomba, Dira za maji 850, Pikipiki 5, uchimbaji na ufukiaji wa mtaro wenye urefu wa mita 23,000, kuunga na kulaza bomba za HDPE 110mm zenye urefu wa mita 17,000, bomba HDPE 63mm zenye urefu wa mita 4,000, HDPE 50mm zenye urefu wa mita 1,200 na HDPE 32mm zenye urefu wa mita 800,” amesema Eng Hamphrey.
Eng Hamphrey ameendelea kusema kuwa, wamejenga vituo 15 vya kuchotea maji ambavyo ni vituo Vitano katika kijiji cha Mwabakima, Jogohya vituo Vinne, Mwamashimba vituo Sita na chemba za maji 22 za dira na valvu.
Amesema jumla ya wateja 90 mpaka sasa wameunganishiwa huduma ya maji majumbani mwao, Vituo 15 vya kuchotea maji katika vijiji hivyo.
MAFANIKIO YA MRADI.
” Wakazi wa vijiji vilivyonufaika na mradi wanapata huduma ya majisafi, salama na yakuaminika kwa muda wote, jambo ambalo limepunguza muda na umbali wa kutafuta na kuchota maji, hivyo itawezesha Wananchi kufanya kazi zingine za maendeleo,” amesema Eng Hamphrey.
ELIMU.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Igunga mjini (IGUWASA) kwa kushirikiana na Mamlaka zingine za Serikali na zisizo za Kiserikali, Ofisi za Vijiji, Mabarozi wa Mitaa, Vyombo vya habari, Shule, Vyuo na Mikutano ya Wananchi wameendelea kutoa elimu mbalimbali ikiwa ni Elimu na umuhimu wa kuunganishiwa maji majumbani, kutumia vituo vya kuchotea maji na kutunza miundombinu yake, Elimu ya kutunza mazingira na upandaji miti pamoja na kutunza vyanzo vya maji katika maeneo yao.
Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Igunga mjini Bernard Kimburey amesema kuwa utekelezaji wa mradi huu unakisi kauli mbiu ya maadhimisho ya wiki ya maji kwa mwaka huu isemayo ” Kuongeza kasi ya mabadiriko katika sekta ya maji kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi,” hivyo utasaidia wananchi kupunguza muda mwingi wa kutafuta maji.
Kwa upande wao Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga na diwani wa Kata ya Mwamashimba Lucas Bugota, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Igunga Nassor Amor, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Igunga Mafunda Ntemanya, Katibu Itikadi na uenezi wa CCM wilaya ya Igunga Peter Kalindo kwa pamoja wamemshukuru Rais Dkt Samia Hassan Suluhu kwa kuwapatia fedha na kuitekeleza Ilani ya CCM kwa kumtua mama ndoo kichwani na kumtua baba ndoo begani kwani sasa watashirikiana na Mamlaka husika kutoa elimu ya utunzaji wa miundombinu hiyo ya maji na vyanzo vingine.
Naye Katibu Tawala wilaya ya Igunga Godslove Kawiche akimwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo Sauda Mtondoo katika uzinduzi na maadhimisho hayo amesema kuwa ni kwa muda mrefu wilaya hii imekuwa na ukame kwa muda mrefu na niwilaya pekee katika wilaya saba za mkoa wa Tabora ambayo kwa mwaka huu imekosa mvua za kutosha kutokana na mabadiriko ya tabia nchi yaliyo sababishwa na ukataji hovyo wa miti.
” Serikali ya awamu ya Sita imedhamilia kumaliza kabisa tatizo hili la maji nchi, ndio maana leo sote tupo hapa kuzindua mradi huu mkubwa wa maji katika vijiji vyetu, na hii ni kutokana na Serikali kudhamilia kumtua ndoo mama kichwani kwa kumsogezea huduma karibu,” amesema Kawiche.
” Niwaombe sasa Wananchi muitunze miundombinu hii ya maji kwani imeigharimu Serikali fedha nyingi zitokanazo na kodi zenu, hivyo niwapongeze IGUWASA na bodi yake kwa usimamizi mzuri wa matumizi ya fedha katika mradi huu,” ameongeza kusema Kawiche.
Akimwakilisha Mkuu wa mkoa wa Tabora,Balozi Dkt Batilda Salha Buriani, Mhandisi wa Majengo mkoa wa Tabora Faustine Ntaray amemshukuru Rais Samia Hassan Suluhu kwa kuendelea kuupatia mkoa wa Tabora fedha za miradi mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu, Barabara, Kilimo, Umeme na Maji jambo ambalo limafanya kupunguza changamoto za kimaendeleo na kiuchumi kwa Wananchi.
” Mradi huu umekuwa mkombozi mkubwa kwa Wananchi wa vijiji vya Mwabakima, Jogohya na Mwamashimba kwani huduma ya majisafi na salama sasa imepatiwa ufumbuzi na itapatikana kwa uhakika, kwani umuhimu wa mradi huu umeonekana na utapunguza usumbufu wa muda wa kwenda kutafuta maji umbali mrefu,” amesema Mhandisi Ntaray.
Amebainisha kuwa, iwapo Wananchi hao na taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali zinapaswa kulipa ankala za maji kwa wakati ili mradi huo uwe endelevu kwani unatoka umbali mrefu katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza, hivyo unatumia umeme kwenye maahine za kusukuma maji hayo, Madwa kuyatibu maji hayo pamoja na gharama za vipuli, hivyo wanatakiwa kulipa ankara za maji hayo mapema.
” Ndugu Wananchi, sekta ya maji ni miongoni mwa sekta za kipaumbele katika mkakati wa kukuza uchumi na kupambana na umasikini, hivyo ujenzi huu ni kutimiza ahadi ya Serikali uliopo katika dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2020/2025, kwamba tutahakikisha kila Mwananchi amepata huduma ya majisafi, salama na ya kutosha kwa gharama nafuu,” amesema Mhandisi Ntaray.
Mhandisi Ntaray, amewaomba Wananchi kutunza vyanzo vya maji pamoja na mradi huo, ikiwa kuacha kuchafua vyanzo hivyo, kukata miti hovyo kwani kufanya hivyo kutaendelea kusababisha janga la ukame na kuleta ukosefu wa maji kwa matumizi ya binadamu ikiwemo kilimo, mifugo, viwanda, uvuvu na uhai wa viumbe hai, kutokana na hayo ameagiza juhudi zifanyike za kuhifadhi vyanzo vya maji katika Halmashauri ya wilaya ya Igunga na za mkoa wa Tabora kwa ujumla.
” Kama mnavyojua mkoa wetu tunakabiliwa na ukosefu wa vyanzo vya uhakika vya maji, Serikali imeamua kuchukua maji Ziwa Victoria umbali wa kilometa 300 ili kuyafukisha maji hayo katika Halmashauri yetu na zingine kwa lengo la kukabiliana na tatizo kubwa la vyanzo vya uhakika vya maji hivyo ni jukumu letu sote kutunza mradi huu na mingine,” amesema Mhandisi Ntaray.
Baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Mwabakima,Editha kiula, ameshukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Hassan Suluhu kwa kuwasogezea huduma ya maji karibu na kuwapunguzia adha ya kutafuta maji umbali mrefu hasa nyakati za usiku.
” Nimeupokea mradi huu kwa shangwe na ndelemo, kwani umetupunguzia adha ya kufuata maji zaidi ya kilometa Saba nyakari za usiku na mchana tulikuwa tunahangaika sana, saizi maji muda unayapata muda wowote iwe saa tano usuku mchana maji unayapata, mimi pia nimeisha unganishiwa maji nyumbani kwangu,” amesema na kuongeza
“Mimi napenda kutoa wito kwa Wananchi wenzangu tuitunze miundombinu mbinu hii ya maji, tutoe taarifa kama maji yanavuja, au kama kuna uharubifu, na kwa mtu atakaye hujumu maji haya tumkamate na kumfikisha katika vyombi husika,” amesema.
More Stories
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni
Tanzania inavyowahitaji viongozi wanawake aina ya Mwakagenda kuharakisha maendeleo
SCF inavyotambua jitihada za RaisSamia mapambano dhidi ya saratani