Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WIZARA ya Madini imesema Sekta ya Madini nchini imeendelea kupiga hatua ambapo maduhuli ya zaidi ya shilingi bilioni 902 sawa na asilimia 90.2 ya lengo la kukusanya Shilingi trilioni moja kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 hadi kufikia leo Mei 15,2025.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo Mei 15, 2025,na Waziri wa Wizara hiyo Anthony Mavunde wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ambapo amesema hiyo ni kabla ya kumalizika kwa Mwaka wa Fedha, huku zikiwa zimesalia zaidi ya siku 45, jambo linalotoa matumaini makubwa kufikiwa kwa asilimia 100 ya lengo.

Waziri Mavunde ameeleza kuwa, Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa ulielekeza Sekta ya Madini ikichangia asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025. Hata hivyo, tayari mwaka 2024 sekta hiyo imefikia mchango wa asilimia 10.1, ikiwa ni mafanikio yaliyotangulia muda uliopangwa.
“Tumefanikiwa kuvuka lengo la kitaifa. Mwaka 2021 Sekta ya Madini ilichangia asilimia 7.3 kwenye pato la Taifa, mwaka 2023 ilifika asilimia 9.1, na hivi sasa tupo kwenye asilimia 10.1 kufikia mwaka 2024. Hili ni jambo la kujivunia,” amesema Mavunde.
Ameeleza kuwa katika kipindi hicho, maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 20, kutoka Shilingi bilioni 623.24 mwaka 2021/2022 hadi kufikia bilioni 753.18 mwaka 2023/2024. Hadi kufikia Mei 9, 2025, Wizara ya Madini ilikuwa imekusanya Shilingi bilioni 902, sawa na asilimia 90.2 ya lengo la mwaka.
“Sekta ya Madini imeendelea kuwa mhimili mkubwa wa upatikanaji wa fedha za kigeni. Mnamo mwaka 2023, mauzo ya madini nje ya nchi yalifikia Dola za Marekani bilioni 3.55, yakichangia asilimia 46.1 ya mauzo yote ya bidhaa nje ya nchi. Aidha, Kampuni za wazawa zimenufaika kwa kiasi kikubwa, ambapo bidhaa na huduma zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.5 sawa na asilimia 92 ya thamani ya manunuzi yote migodini zilitolewa na Watanzania,”amesema Mavunde.

Vilevile amesema Wizara ya Madini imeendelea kuimarisha mazingira ya biashara ya madini kwa kuongeza idadi ya masoko na vituo vya ununuzi hadi kufikia 152 nchi nzima. Aidha, minada ya madini ya vito imeanzishwa upya baada ya kusimama tangu mwaka 2017. Mnada wa kwanza ulifanyika Desemba 2024 na wa pili Aprili 2025, ambapo madini yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.5 yaliuzwa na kuiwezesha Serikali kukusanya zaidi ya Shilingi milioni 163 kupitia mrabaha, ada za ukaguzi, usimamizi na ushiriki wa minada hiyo.
Katika kuwajengea mazingira bora wachimbaji wadogo,Mavunde amesema Serikali imefuta leseni na maombi 2,648 ambayo hayakuendelezwa na ina mkakati wa kuzigawa upya kwa wachimbaji wadogo.
Aidha,amesema STAMICO imeendelea kuwalea wachimbaji hao kupitia vituo vya mfano na mitambo ya CIP, huku Kamati maalum ya watu 6 ikiundwa kwa ajili ya kuishauri Serikali kuhusu njia bora za kuwawezesha wachimbaji hao. Pia, mfumo wa dhamana (Credit Guarantee Scheme) umeandaliwa, sambamba na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuchakata chumvi kwa ajili ya kusaidia wakulima wa chumvi nchini.
Vilevile amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dkt. Samia, Jumla ya leseni za Uchimbaji Mkubwa, wa Kati na Mdogo 34,348 zimetolewa na Kampuni mbalimbali zimesaini mikataba kwa ajili ya kuanza uendelezaji wa migodi nchini.
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) nalo limepiga hatua kubwa, kutoka kutengeneza faida ya shilingi bilioni 1 kwa mwaka hadi kufikia bilioni 84 kwa mwaka ndani ya miaka mitatu.

More Stories
SGR yaiweka Tanzania Katika Ramani ya Usafirishaji wa Kisasa
Dkt.Jafo:Fufueni viwanda kabla serikali haijaingiza mkono wake
Waziri Mkuu atembelea Kituo cha Kuhifadhi Data Kimtandao NIDC.