January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sekta ya afya na juhudi madhubuti za Rais Samia

Na Markus Mpangala,Timesmajira,Online,Mtwara

KUTOKA Mkoani Mtwara hadi Wilaya ya Nyasa iliyopo Mkoa wa Ruvuma ni umbali wa kilometa 800.

Umbali kutoka Mkoa wa Mtwara hadi Dar Es Salaam ni takribani kilometa 400. Hali kadhalika umbali kutoka Dar Es Salaam hadi mkoani Ruvuma ni takribani kilometa 1,000 kwa kutumia njia ya Mtwara-Masasi-Tunduru hadi Songea.

Lakini endapo ukitumia barabara ya Dar es Salaam-Morogoro-Iringa-Njombe hadi Ruvuma wastani wa kilometa 900. Ukitafsiri takwimu hizi utaona kuwa umbali huo unaweza kumlazimisha mgonjwa mmoja kutoka Songea kufuata huduma mkoani Dar es Salaam, mfano matibabu ya saratani.

Magonjwa mengine ambayo hushindikana kutibiwa katika baadhi ya hospitali huwalazimisha wananchi kufuata huduma hiyo kwenye hospitali kubwa.

Kwa kuona changamoto hiyo, Serikali ya awamu ya sita imefanikiwa kuwasogea huduma za afya wananchi wa mikoa ya Kusini na Nyanda za Juu kusini.

Rais Samia na Serikali yake kwa juhudi na maarifa kupitia Wizara ya Afya, Jinsia na Watoto imekuwa kielelezo cha kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kote nchini.

Kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake Rais Samia amefanikisha ujenzi wa Hospitali mbalimbali ambako Serikali imebainisha mkakati wake ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za Afya kwa uhakika maeneo ya karibu yao.

Miongoni mwa fursa zilizotengenezwa na Serikali ni mradi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda iliyozinduliwa na Rais Samia mwenyewe huko mkoani Mtwara.

Pongezi hizo ziende pamoja na wadau wote walioshiriki kuwezesha na kusogeza huduma za afya kwa wananchi wetu kote nchini. Hospitali ya Kanda ya Kusini inatajwa kuwa muhimu si kwa wakazi wa Lindi na Mtwara pekee bali pia wengine kutoka Wilaya za Tunduru na Namtumbo.

Pia ifahamike Tanzania ilianzisha mradi wa Mtwara Corridor ambao ulihusisha ujenzi wa barabara kutoka Mtwara hadi Bandari ya Mbamba Bay kwa kiwango cha Lami.

Hali kadhalika ilikuwa kuimarisha hali ya Bandari ya Mtwara pamoja na ujenzi wa Reli hadi Mbamba Bay.

Hatua ya pili baada ya barabara ya lami imezinduliwa sasa kwa huduma ya afya. Hivyo basi, mradi wa Hospitali ya Kanda ya Kusini ni hatua ya pili ambayo imewezesha wakazi wa Mikoa husika kupata matibabu kutoka kwa wataalamu bingwa na waliobobea.

Hatua hiyo inapaswa kupongezewa kwa nguvu zote kwa sababu jamii zetu za Kitanzania upo utamaduni kwa baadhi kuamini katika ushirikina na uchawi pale zinaposhindwa kung’amua aina za magonjwa yanayowasumbua.

Katika jamii za Kanda ya Kusini na Nyanda za Juu Kusini kumekuwa na kasumba kuwa magonjwa yasiyofahamika yanapokatisha uhai wa watu hudaiwa kuwa ni vifo vya uchawi na ushirikina.

Baadhi ya watu hudhani kuwa magonjwa kama saratani hayatibiki na huambatana na imani kuwa mgonjwa husika amerogwa au kuchezewa kishirikina na uchawi.

Si siri jamii yetu imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya huduma ya afya kutokana na elimu duni juu ya magonjwa, vifaa bora, wauguzi, madaktari bingwa na waliobobea pamoja na vituo vya Afya.

Katika mazingira tuliyonayo tunapoona Hospitali kubwa ya Kanda ya Kusini iliyozinduliwa na Rais Samia mwenyewe na kuanza kutoa huduma maana yake tunapunguza kiwango fulani cha imani za kishirikina.

Ni rahisi jamii kuamini mtu akifariki ghafla kwa kuzidiwa na ugonjwa kama Malaria kuwa amerogwa na wachawi, lakini si rahisi kukiri wana upungufu wa ufahamu kuhusu magonjwa.

Mafanikio ya kujenga Hospitali za Kanda yanapaswa kuepeleka pongezi kwa Serikali ambayo imethubutu na kuendelea kuongoza njia namna bora ya kushughulikia matatizo ya wananchi.

Muonekano wa Hospitali ya Kanda ya Mtwara

Jitihada za kuimarisha hali ya afya nchini ndiyo husukuma viongozi kusimama kidete na kuhakikisha kila kaya inapata huduma za afya zilizo bora pamoja na kuondokana na imani za kishirikina na uchawi.

Wataalamu wa uchumi wanatuambia kuwa jamii yenye afya ndiyo yenye mchango mkubwa wa kujenga uchumi wa Taifa. Kwamba afya dhaifu huchangia watu dhaifu na kuchochea uchumi wa shelabela. Ili nchi ijiongezee nguvu katika maendeleo ni lazima maarifa ya watu wenye afya bora yatumike ipasavyo.

Kwa hiyo uamuzi wa serikali ya awamu ya sita kuhakikisha inaongeza nguvu katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi kuanzia ngazi ya mtaa, Kijiji,Kata,Tarafa,Wilaya,Mikoa,Kanda hadi Taifa ni jambo linalopaswa kuipa kongole.

Katika mpango huo wa kutoa huduma bora za afya zitawezesha kuongeza kiwango cha ufahamu juu ya magonjwa na afya kwa ujumla miongoni mwa wananchi.

Wananchi watapata fursa ya kuzifanya Hospitali kuwa kimbilio kuliko kuamini ushirikina na uchawi katika kutafuta tiba za magonjwa.

Nchi yetu imeshuhudia kuwa sehemu ya wimbi la mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO ambao haukujulikana. Ili kuwaondolea elimu hafifu, juhudi za kuelimisha wananchi kupitia ujenzi wa miradi ya Hospitali ambako watapata kuwa karibu na wataalamu wa afya.

Serikali ya awamu ya sita imeonesha kuwa inao wajibu wa kuwapunguzia wananchi wake hisia za imani za kishirikina na uchawi pale magonjwa wasiyoyajua yanapowaelemea, ili wafahamu ni aina mojawapo ya maradhi yanayowakumba binadamu.

Hatukujua ugonjwa wa Kimeta, lakini wananchi waliambiwa na elimu ikasambazwe pamoja na miradi ya vituo vya afya kuongezwa. Hatujajua ukali wa saratani, lakini wananchi wanaelimishwa na kujua si uchawi.

Rais Samia Suluhu Hassan akisikiliza maelezo kuhusiana na huduma zinazotolewa na Hospitali hiyo

Hatukujua madhara makubwa ya ugonjwa wa Malaria ambao huweza kuua ghafla, kwa sababu tuliamini katika ushirikina na uchawi. Hata hivyo suluhisho linaonekana dhahiri kwa kipindi cha miaka miatatu ya kuongoza nchi yetu serikali ya awamu ya nne imefanikisha kusogeza huduma za Afya kwa wananchi wa Mikoa ya Kusini na kuwafanya wapige vigelegele na nderemo pamoja na kuishukuru serikali.

Serikali ya awamu ya sita iendelee kuwa na wajibu wa kusambaza tabasamu kwa wananchi katika sekta ya afya.
Baruapepe; mawazoni15@gmail.com

=========================