Na Mwandishi wetu, TimesMajira online
Tanzania ni mahali salama, ina maeneo mazuri kwa ajili ya uwekezaji hivyo kufanya kuwa ni fursa kubwa ya kuwekeza hususani kwenye sekta ya afya.
Akiongea na Wadau wa sekta binafsi na mashirika ya kidini nchini, Prof. Abel Makubi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto leo jijini Dodoma amesema kuwa ni wakati sasa wa sekta binafsi kujikita kuwezekeza kwenye sekta ya afya kulingana na mazingira wezeshi yaliyopo ambayo yatasaidia kuleta maendeleo ya nchi.
“Nchi yetu ya Tanzania ni eneo salama na kuna mazingira mazuri ya uwekezaji,Watanzania, Wafanyabiashara na wawekezaji binafsi bado mna nafasi nyingi ya kuwekeza kwenye sekta ya afya kuliko kuiachia Serikali peke yake “.
Prof. Makubi amesema kuwa sekta ya afya inajihusisha na utoaji wa huduma kwa wananchi lakini ni eneo la fursa la uwekezaji na kama serikali wameona ipo haja ya kuwaita na kuongea na wadau wa sekta binafsi ili kuangalia uwekezaji zaidi ili kuleta maendeleo makubwa katika huduma za tiba, viwanda vya madawa pamoja na vyuo vya mafunzo vya wataalam wa afya.
“Tunahitaji sana wataalamu wa afya na tunaona hivi sasa kuna vyuo vingi vya mafunzo vya wataalamu wa afya ambavyo vinamilikiwa na mashirika ya dini na sekta binafsi, hivyo kama serikali tunawashukuru kwani wanasaidia katika kuwahudumia wananchi wetu”Aliongeza Prof. Makubi.
Hata hivyo Katibu Mkuu huyo amesema kikao hicho wameona yapo maeneo mbalimbali ambayo yanaweza kuwekewa mkazo wa kuwekeza akitolea mfano viwanda vya madawa, hospitali na vituo vya kutolea huduma katika sehemu mbalimbali za nchi.
“Mfano kuwekeza Mikoa ya Magharibi au kusini inawezekana kwani kule mtwara tumejenga hospitali kubwa ya kanda mnaweza kuanzisha kiwanda na hivyo kutoa huduma hata nchi za jirani, na tunapoelekea kwenye matibabu ya kitalii (Medical Tourism) kule Arusha kwenye watalii wengi mnaweza kuwekeza hospitali kubwa ambayo itawahudumia, tunazo fursa nyingi njoo muwekeze” Alisistiza Prof. Makubi.
Kwa upande wa mapambano dhidi ya UVIKO-19 Prof. Makubi aliwashukuru sekta binafsi katika kushirikiana kwenye kutoa elimu na kuhamasisha wananchi katika kuchanja chanjo dhidi ya ugonjwa huo.
“Tunatambua sekta binafsi mlivyoshughulika katika mapambano ya ugonjwa huu toka wimbi la kwanza,ya pili na hata la tatu tunawashuru ila pia tunawaomba muendelee kushirikiana katika kuhamasisha wananchi ili kwa hiara yao waweze kuhamasika na kujitokeza kucghanja.
Prof. Makubi amesema wananchi wakichanja kwa asilimia kubwa na kwa muda mfupi wananchi watakuwa wamejanga kinga ya umoja ya jamii na hivyo kupunguza maambukizi na hata kuondoa kabisa ugonjwa huu ambao umeathiri dunia nzima.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato