Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Husna Sekiboko amesema atakwenda kumuona Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) riziki Shemdoe ili atoe sh. 63,428,834 kwa ajili ya kukamilisha Jengo la Dharura (EMD) katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, Magunga.
Sekiboko amesema pamoja na Serikali kujenga majengo ya aina hiyo karibu nchi nzima, ameitaka TAMISEMI kuchukulia kwa uzito wa pekee jengo hilo katika Hospitali ya Magunga sababu lipo njia kuu ya Dar es Salaam- Arusha, na ndiyo lilikuwa mkombozi kwa majeruhi wa ajali ya Coaster iliyotokea Kijiji cha Magila- Gereza Februari 3 saa 4.30 usiku Februari 3, mwaka huu, ambapo watu 20 walipoteza maisha.
Sekiboko aliyasema hayo Februari 21, 2023 baada ya kufika kwenye Hospitali ya Magunga akiwa kwenye ziara ya kutembelea miradi na kuzungumza na wananchi katika Mkoa wa Tanga, ambapo anatembelea tarafa zote za Mkoa wa Tanga zenye kata 245.
“Mimi, Katibu Mkuu Shemdoe ni kaka yangu, hivyo nitakwenda kumueleza atoe kiasi hicho cha fedha sh. milioni 60 ili kukamilisha jengo hili. Najua Serikali ya Mama Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inafanya kazi kubwa, na imejenga majengo kama haya karibu nchi nzima, lakini kwa Hospitali ya Magunga, korogwe, jengo hili ni muhimu sana sababu ndiyo tegemeo kwa barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi na Arusha, hasa inapotokea ajali.
“Kama Mganga Mkuu wa Halmashauri alivyosema, wale majeruhi wa coaster waliokuwa wanasafirisha mwili, waliweza kutibiwa hapa, hivyo ni namna gani TAMISEMI wanatakiwa kuchukua hili jambo kwa uzito wa pekee” alisema Sekiboko, na kuelezwa hata Shemdoe alishafika kwenye jengo hilo kwa ajili ya kulikagua.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Korogwe (TMO) Vendavenda Sumuni (sio daktari), alisema wanahitaji sh. 63,428,834 ili kukamilisha ujenzi wa Jengo hilo la EMD, ambapo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 96, na limeanza kutoa huduma tangu Januari 24, mwaka huu, ambapo hadi kufikia Februari 20, mwaka huu, wateja 81 wamepata huduma katika jengo hilo, ambapo wanaume ni 36 na wanawake 45.
“Moja ya changamoto kwenye Jengo la Dharura ni fedha za umaliziaji baadhi ya huduma ikiwemo kuweka A/C (viyoyozi), kuweka sinki la choo cha walemavu na chumba cha kutakasia vifaa (sluice room). Pia kujenga walk way (njia ya kutoka jengo moja kwenda jingine), na uwekwaji wa vigae (concrete tiles) eneo la kuingilia gari la wagonjwa.
“Lakini changamoto ya pili ni watumishi. Jengo hili linahitaji watumishi 40, ambao watafanya kazi bila kuingilia maeneo mengine ya Hospitali ya Magunga, lakini hadi sasa kuna watumishi sita tu. Japo kuna jitihada tumefanya, tumepeleka wataalamu 20 kupata mafunzo ya kuhudumia majeruhi kwa ajili ya jengo hili tu” alisema Sumuni.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo hilo kwa Mbunge, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Magunga Dkt. Elisa Elisante alisema ujenzi ulianza Machi 21, 2022 na kutekelezwa kwa Force Account kwa kutumia local fundi, ambapo makadirio ya awali ya Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ilikuwa lijengwe kwa sh. 387,580,020.
“Ujenzi wa mradi huu ulianza rasmi Machi 21, 2022 kwa kutumia local fundi, na mradi ulipaswa kutekelezwa kwa siku 90 hadi Juni 20, 2022. Hata hivyo, kwa changamoto mbalimbali ililazimu fundi kuomba kuongezewa siku 45 hadi Agosti 5, 2022. Aidha, fundi amekuwa akiomba nyongeza ya muda kadri fedha unapopatikana, ambapo hadi sasa mradi upo kwenye hatua ya umaliziaji.
“Mradi huu umetumia sh. 330,180,000, ambapo sh. milioni 300 ni fedha za UVIKO 19 kutoka Serikali Kuu na sh. 30,180,000 ni fedha kutoka Mapato ya Ndani ya Halmashauri ya Mji Korogwe. Kiasi cha sh. milioni 68.4 ni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya ujenzi” alisema Dkt. Elisante.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini