Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM
KAMPUNI ya Serengeti imeahidi kuendelea kuwasaidia wanafunzi katika tasnia ya utalii kupitia mradi wake wa ‘Learning for Life’ ambao unawawezesha wanafunzi wasiojiweza kupata msaada wa kifedha ili kugharimia masomo yao ya elimu ya juu.
Mpango huo unaotarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha wa 2024/25 ni sehemu ya nguzo ya Ushirikishwaji wa SBL, ambayo imejikita kushirikisha makundi yanayosahaulika kushirkishwa kwenye shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumzia mpango endelevu wa SBL kwenye uwekezaji katika elimu, Meneja Mawasiliano na mambo Endelevu wa SBL, Rispa Hatibu amesema chini ya nguzo Endelevu ya SBL, kampuni ya Serengeti imejumuisha elimu kama moja ya vipengele muhimu vinavyojulikana kama ‘Learning for Life’ ambapo SBL atawekeza kwenye sio tu kusaidia wanafunzi katika masomo ya kilimo na kozi za STEM lakini pia sekta zingine ambazo ni muhimu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Chini ya mpango wa ufadhili wa ‘Kilimo Viwanda’, SBL imekuwa ikitoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka jamii za wakulima wanaotaka kusoma masomo ya kilimo. Tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 2020, zaidi ya wanafunzi 200 kutoka jamii za wakulima wamenufaika na mpango wa ufadhili wa masomo.
“SBL, tunasimamia uendelevu, kila kitu tunachofanya kuanzia kwenye biashara hadi uwekezaji wetu katika jamii, tunajitahidi kufanya vitu kwa uendelevu. Ni kwa sababu hii kwamba tumechukua mtazamo sawa linapokuja suala la uwekezaji wetu katika elimu, kwa hivyo neno ‘Kujifunza kwa Maisha’. Kupitia mpango huu tunajipanga kupanua uwekezaji wetu katika elimu kwa kutoa msaada wetu kwa tasnia ya utalii, kuanzia mwaka wa fedha wa 2024/25,” amesema Hatibu.
Amesema kufuatia mafanikio ya uwekezaji wa miaka 4 katika elimu kupitia mpango wa ufadhili wa Kilimo Viwanda na uanagenzi wa STEM ambao umenufaisha mamia ya wanafunzi na wahitimu, SBL iliona umuhimu wa kutoa msaada wa kifedha kwa wanafunzi katika masomo ya utalii,
“katika miaka minne iliyopita. tumekuwa tukiwasaidia wanafunzi katika kozi za kilimo na sayansi, na mwaka ujao wa fedha, tutapunguza kidogo uwekezaji wetu katika programu kama Kilimo Viwanda, na ingawa tutaendelea kuunga mkono juhudi katika sekta hizi mbili, tulitaka kuongeza msaada katika sekta ya utalii pia, kwa kuzingatia kwamba hii ni moja ya sekta muhimu zinazochangia kiasi kikubwa katika uchumi wa nchi yetu na uboreshaji wa maisha.”
Hatibu amebainisha kuwa, mwaka ujao wa fedha unapokaribia, SBL itafichua maelezo zaidi kuhusu mpango wake wa ‘Kujifunza kwa Maisha’ katika tasnia ya utalii ikiwa ni pamoja na vipimo vya vigezo vya kunufaika na programu hiyo, idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa kufaidika nayo pamoja na vyuo na wadau wengine wakuu ambao SBL itashirikiana nao ili kutekeleza mpango huo kwa mafanikio.
Kando na kuwekeza katika elimu katika mwaka ujao wa fedha, SBL itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ya jamii ambayo imepachikwa kwenye mpango wake wa Society 2030: Spirit of Progress. Hii itahusisha kuwekeza katika miradi ya maji kupitia nguzo yake ya ‘Maji ya Uhai’ pamoja na kuwekeza katika ajenda yake ya uendelevu.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam