December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sayansi, teknolojia na ubunifu kuchochea maendeleo ya uchumi nchini

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu yanachochea kasi maendeleo ya uchumi nchini.

Prof. Mkenda ameyasema hayo Aprili 28, 2023 jijini Dodoma katika kilele cha Wiki ya Ubunifu kitaifa ambapo amesema sayansi, teknolojia na ubunifu zina mchango mkubwa wa kuchagiza maendeleo ya kiuchumi na kwamba nchi mbalimbali zimefanikiwa kutokana na kuwekeza kwenye eneo hilo.

“Ibara ya 102 ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inaahidi kuwa Serikali itahakikisha inaendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu, tunachokifanya hapa leo ni kuendeleza yale ambayo chama chenye Serikali kilitoa ahadi wakati wa kuomba kura kwa wananchi. Baada ya kufanya maonesho haya na MAKISATU tunaona sasa tunapata bidhaa zilizoibuliwa, zimebiasharishwa na ni jukumu letu kuzitangaza,” amesema Prof Mkenda.

Ameongeza “Nchi ya Norway iliendelea kwasababu iliwekeza kwenye elimu hasa sayansi, teknolojia na ubunifu na nchi nyingine nyingi zimeendelea kwasababu hii kuwezesha sayansi na teknolojia na baadae kuziingiza teknolojia zao sokoni, tusidhani suala hili ni dogo wote walioanza na ubunifu walianza kwa kubezwa zamani miaka ya 50 magari ya Japan yalikuwa yakibezwa leo hii barabarani magari mengi ni ya Japan.” ameongeza Prof. Mkenda

Waziri Mkenda ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau mbalimbali walioshiriki katika kuhakikisha wiki ya Ubunifu Tanzania inafanikiwa.

“Niwashukuru wadau mbalimbali ambao wameungana nasi kufanikisha maonesho haya napenda kutoa shukrani za pekee kwa UNDP na wadau wengine kwa kutushika mkono kupitia program ya FUNGUO, benki ya NMB, CRDB, UNESCO, WFP, LM International na TANZTECH ambao wataanza kuzalisha vishikwambi nchini na wataungana na sisi kupitia vyuo mbalimbali ili kusaidia wanafunzi wetu kuingia kwenye mafunzo maalum ya masuala ya kielektroniki na uhandisi,”amesema Prof. Mkenda

Amesema moja ya mambo ambayo Serikali inafanya ni pamoja na kuhimiza vijana kusoma sayansi ili kupata wataalamu wa kutosha kwenye fani za sayansi na uhandisi.

“Bunge liliidhinisha fedha za kutoa ufadhili huo si mkopo na tunaita ‘Samia Scholarship’ kwa ajili ya kusomesha wanasayansi tunataka tuwe na wabobezi kwenye sayansi ili watakapokwenda kufanya shughuli za kisayansi watasaidia kuendeleza teknolojia itakayotusaidia kwenda kwenye ubunifu, kwa hiyo wanafunzi wetu wa kidato cha sita ambao wamefanya vizuri kwenye masomo ya sayansi wakisoma uhandisi, udaktari wanapata ufadhili huu,”amesema Prof. Mkenda

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof.Carolyne Nombo, amesema maadhimisho yq Wiki ya Ubunufu ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuongeza hamasa ya matumizi ya sayansi na teknolojia na ubunifu kama nyenzo muhimu ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Amesema tangu kuanzishwa kwa Mashindano ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) Mwaka 2019 wabunifu na wavumbuzi wachanga wapatao 2,636 waliibuliwa na kutambuliwa na Wizara.

“Wabunifu wengine 283 wanaendelezwa na Serikali kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili ubunifu wao ufikie hatua ya kuwa bidhaa na kuingia sokoni ili kuongeza fursa ya ajira na vipato kwa vijana wetu, wabunifu wachanga wanaendelezwa kwenye vituo atamizi na kumbi za ubunifu ambazo hadi sasa bunifu na teknolojia 53 zimefanikiwa kufikia hatua ya kuwa bidhaa na hivyo kutumika kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya kilimo, maji , madini, afya, elimu,”amesema Prof. Nombo.

Amebainisha moja ya changamoto inayowakabili wabunifu wachanga ni kukosa mahali pa kuendeleza bunifu zao na kwa kutambua hilo serikali kupitia taasisi ya COSTECH imeanzisha kumbi za ubunifu na atamizi za DTB kwa lengo la kuendeleza vijana wenye mawazo ya ubunifu mbalimbali.

“Kuwepo wa kumbi hizi umechochea wadau Sekta za umma na bunifu kuanzisha kumbi za ubunifu na teknolojia zaidi ya 50 ili kuendeleza wabunifu wachanga, Serikali kupitia Buni Hub na DTB imewezesha kuanzishwa kwa kampuni changa mapya zaidi ya 94 na kutoa ajira na ajira zisizo za moja kwa moja kwa vijana zaidi ya 30,000 mchango wa kampuni hizo kwenye pato la Taifa ,”amesema Prof. Nombo.

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko amepongeza Wizara ya Elimu kwa kuendeleza ubunifu na ugunduzi hali itakayochagiza kufikia Tanzania ya Viwanda.