January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SAU kununua ndege ya abiria kwa kila mkoa

Na Rose Itono,TimesMajira Online,Dar

CHAMA cha Sauti ya Umma (SAU) kimezindua Ilani na kampeni zake kwa ajili uchaguzi unaotarajia kufanyika Oktoba 28, mwaka huu, huku kikiahidi kuwa endapo kikishika dola huo utakuwa mwisho ma matumizi ya jembe la mkono nchini na kila mkoa utakuwa na ndege yake kwa ajili ya kubeba abiria.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ilani na kampeni za chama hicho jana, jijini Dar es Salaa, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Muttamwega Mgaywa alisema ilani ya chama hicho imelenga kuikomboa nchi kupitia kilimo na viwanda.

Alisema chini ya uongozi wa Serikali ya SAU, hakuna mkulima atakayelima Kwa kutumia jembe la mkono, badala yake trekta ndizo zitakazotumika ili kumpunguzia mzigo kwa mkulima.

Pia aliahidi kuwa chini ya Serikali ya chama hicho, wanawake watakuwa wakijifungua bure. Wakati wa uzinduzi huo mgombea urais SAU na mgombea mwenza, Satia Mussa waliwasha trekta kuashiria uzinduzi wa matukizi ya trekta kwenye shughuli za kilimo kama ishara ya mwisho wa kilimo cha kutumia jembe la mkono.

“Chama chetu kina sera mbadala hakipo kwa ajili ya kupinga kila maendeleo yaliyofanyika badala yake kimelenga kuyapeleka mbele kwa kasi,” alisema Mgaywa na kuwawataka Watanzania ifikapo Oktoba 28, kuwachagua wagombea wote wa chama hicho kuanzia urais, ubunge na madiwami.

Kwa upande wake, Mussa (mgombea mwenza) aliwaahidi wanawake nchini kwamba watawatua mzigo wanapokwenda hospitali kwa ajili ya uzazi, kwani chama hicho kitatoa huduma zote bure hospitalini.

Naye Mkurugenzi wa Propaganda, Kunje Ngombale Mwiru akifafanua mpango wa chama hicho kutoa usafiri wa ndege ya abiria kila mkoa, alisema kuwa hakuna kinachoshindikana, kwani nchi ina rasilimali za kutosha.

Katibu Mkuu wa Chama hicho, Majalio Kyala aliwataka Watanzania kuwachagua wagombea wa SAU ili kuleta nafuu ya maisha kwa Watanzania kupitia kilimo.

Aliwaahidi wanawake na wajasiriamali nchini kupata mitaji ya sh. milioni moja kila mmoja kwa ajili ya kuinua mitaji yao.

Kyala alisema sera za SAU zimelenga kumshibisha kila Mtanzania kupitia kilimo sambamba na kuhakikisha viwanda vinakuwa vya kutosha ili kumuwezesha kila kijana wa Kitanzania kupata ajira.

MWISHO