December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SAU: Ikulu sio mahali pa kuchezea au kuingia mchoyo

Na Rose Itono, TimesMajira Online, Dar es Salaam

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU) Mutamwega Mgaywa, amesema Ikulu si mahali pa kuchezea wala kuingia mtu mchoyo badala yake wanatakiwa kuingia watu waadilifu na wazalendo.

Akizungumza wakati akinadi sera za chama chake maeneo ya Kivukoni Manispaa ya Ilala jana, Mugaya amesema akichaguliwa na kuwa rais wa nchi hii atahakikisha kila Mtanzania anaishi maisha bora.

Amesema kutokana na uadilifu na uzalendo alionao ana kila sababu ya kuwa rais wa nchi hii ili aweze kumaliza changamoto za wananchi.

“Kupitia uadilifu nilionao sitakuwa mchoyo kila Mtanzania ataishi maisha bora,”amesema Mgaywa na kuongeza kuwa kupitia benki ya wajasiriamali atakayoianzisha atapata mtaji wa sh. milioni 1 ili akuze biashara.

Aidha, amesisitiza wapiga kura kumchagua ili aweze kulitumikia taifa kwa uadilifu, kwani hakuwahi katika utumishi wake katika nchi hii hajawahi kuomba kutoa wala kupokea rushwa.

Naye mgombea mwenza wa urais kupitia chama hicho, Satia Mussa Bwera ameahidi kushughulikia kero zote za wanawake ikiwa ni pamoja na kutoa taulo za kike bure.